Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
TUME ya Ushindani nchini (FCC) imesema itaendelea kulinda wananchi ili wasiuziwe bidhaa zisizo na ubora na bandia kwakusimamia sheria ya ushindani inayodhibiti bidhaa hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Mkurugenzi Mtendaji wa FCC, William Erio amesema FCC itahakikisha mwananchi yeyote haumizwi na bidhaa zisizo na ubora kupitia sheria ambazo zimewekwa.
“FCC itahakikisha mwananchi yeyote haumizwi na bidhaa zisizo na ubora ikiwemo kusimamia sheria ya ushindani nchini inayodhibiti bidhaa hizo,pia tutaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kuhusu bidhaa bandia ,”amesema Erio.
Amesema FCC imejitahidi kutoa elimu kwa wafanyabiashara juu ya kuepuka bidhaa bandia.
Erio amewahakikishia wawekezaji kuwa Tanzania ni sehemu sahihi kwa uwekezaji kutokana na sera nzuri ikiwemo kuwepo kwa Mamlaka inayodhibiti bidhaa bandia
“Majukumu yetu pia ni kutoa elimu kwa watu kutokufanya Biashara Bandia na kuharibu ushindani wa biashara, sisi FCC tutaendelea kuchukua hatua kwa yeyoye atakayebainika kufanya hivyo,”amesema Erio.
Erio amewataka wafanyabiashara na wawekezaji kabla ya kufanya biashara nchini watembelee FCC kwa lengo la kupata elimu .
“Na sisi tunatumia maonesho haya pamoja na kueleza kazi kwa Umma,tunatumia maonesho haya pia kunawashauri kutofanya Biashara Bandia pamoja kutoweka bei kubwa itakayomuumiza mlaji,”
“Tunawakaribisha kwenye Banda hili, tutatoa elimu kipindi chote cha maonesho, hivyo niwakaribishe Wafanyabiashara na wananchi Kwa ujumla waweze kutembelea banda letu,” amesema Erio.