Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WAFANYABIASHARA wametakiwa kutembelea katika viwanja vya maonesho ya 48 ya biashara ya Kimataifa ili kuweza kuona teknolojia mbalimbali zikiwemo za kilimo na madini ambazo zitawasaidia kukuza biashara zao.
Akizungumza katika tamasha la siku maalum ya Iran ikiwa ni muendelezo was nchi mbalimbali kujitangaza katika viwanja vya Sabasaba ,Mkurugenzi Mtendaji Tanzania Chember Of Commerce Industry and Agriculture(TCCIA) Oscar Kisanga amesema tangu maonesho yaanze amekuwa akifuatilia siku hizi maalum za nchi mbalimbali na kugundua kuwa biashra zinahitaji teknolojia.
“Nimejifunza biashara huwezi kufanya peke yako lakini pia biashara inahitaji teknolojia ,kwa kweli teknolojia haiepukiki,nimeangalia s Japan Day,Korea Day ,China Day wapo katika fani zote zikiwemo kilimo na madini,”amesema Kisanga.
Amesema teknolojia ni jambo la muhimu ambalo Watanzania wanapaswa kubadilishana n ujuzi na ufahamu na watu wa nchi hizo.
Amesema siku ya Iran wameipokea kwa mikono miwili ambapo kwa upande wao kama TCCIA wameona kuna fursa nyingi kutoka nchi hiyo ikiwemo kilimo na mambo ya madawa.
“Lakini wapo vizuri pia katika masuala ya utafiti na maendeleo hasa katika dawa za kilimo na binadamu kwa hiyo mimi kama mkurugenzi natoa wito kwa watanzania wote lakini pia kwa wanachama wetu tushirikiane na wafanyabiashara hawa ili kuangalia namna gani tutafanya kazi ,”amesema Kisanga.
Amesema hakuna mtu anayeweza kufanya biashara peke yake hivyo ni vema kuunganisha nguvu kwa nchi kama Iran ili kuongeza mtandao wa kibiashara na kufikia malengo.
Kwa upande Mkurugenzi wa Tantrade, Latifa Khamis amesema leo imekuwa ni siku nzuri sana kwa sababu nchi hizi mbili, zimeonyeaha Ushirikiano mkubwa wa kibiashara,na kupelekea wafanyabiashara kunufaika kwa kuwa bidhaa ambazo zinatoka Tanzania zinapelekwa Iran na za Iran zinaletwa Tanzania hivyo kuleta tija katika ukuaji wa uchumi wa nchi hizi mbili.
“Tumejifunza mengi sana kwa wenzetu hawa wa Iran ambao kiukweli wako vizuri sana kwenye mambo mbalimbali kama vile tulivyojionea upande wa madawa yao ya kupambana na sumu za viumbe hatari kama vile nyoka, nge na viumbe wengine hatari”,
“Pia kwenye baadhi ya sekta ya masuala ya afya,wana chanjo kwa hiyo kampuni kubwa za Iran wanaotengeneza chanjo kubwa kubwa wanatafuta washirika hapa Tanzania hasa wa serikali ili kuhakikisha ile teknolojia wanaileta hapa watengeneze chanjo na hatimaye kuuuza nje,”amesema Latifa.
Katika tamasha hilo watu wa Iran walionesha vitu vyao mbalimbali vya kitamaduni ikiwemo madawa, vyombo vya nyumbani na mengineyo.