Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema matumizi ta gesi asilia kwenye magari yameendelea kuongezeka ambapo mpaka sasa takribani magari 5,000 yamefungwa mfumo huo.
Akizungumza katika banda la Ewura lililopo katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere Mkurugenzi Mkuu wa Ewura Dk.James Andilile amesema matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaongezeka siku hadi siku.
“Matumizi ya gesi asilia kwenye magari yanaongezeka tuna takribani magari 5000 ambayo yanatumia gesi asilia hii imetusaidia sana kupunguza matumizi ya dola katika kuagiza nishati ya mafuta kutoka nje,”amesema Dk.Andilile.
Amesema matumizi ya dola yamepungua kwa sababu gesi inayotumika katika magari inapatikana ndani ya nchi.
Amesema kutokana na kasi ya kuongezeka kwa matumizi ya gesi kwenye magari ametoa rai kwa wawekezaji kuwekeza katika ujenzi wa vituo vya kuuza gesi.
“Naendelea kuwahamasisha baadhi ya wawekezaji katika ujenzi wa vituo tunawakaribisha nawaahidi tukipata maombi yao tutayashughulikia kwa haraka kwa sababu tunataka wananchi ambao wametuweka katika nafasi tulizonazo waweze kupata huduma hizi katika ubora unaotakiwa,”amesema Dk.Andilile.
Kwa upande wa maji amesema wanaendelea kusimamia suala la upatikanaji wa huduma za hiyo kila eneo huku serikali ikiendelea kufanya uwekezaji.
“Ni wajibu wetu wa kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na serikali utawezesha kupata huduma endelevu katika maeneo husika na ni wajibu wetu pia kuhakikisha ubora wa huduma unaimarika na uwekezaji,”amesema Dk.Andilile.
Akizungumzia kuhusu mafuta amesema wanaendelea kuimarisha suala la ubora ambapo kufikia Juni 30 takwimu zilikuwa zinaonyesha ubora wa mafuta ulikuwa umefikia asilimia 97.
“Mafuta yanauzwa kwa kiwango cha ubora,pia kwenye bei tunaendelea kufuatilia mwenendo wa bei kwenye soko la Dunia ili kuhakikisha kwamba kuna unafuu wowote uliopo kwenye soko la dunia lazima uonekane na katika soko la ndani,”amesema Dk.Andilile.
Amesema mamlaka imeendelea kutoa bei za kila mwezi kulingana na soko la Dunia.