Na Mwandishi Wetu ,Dar es Salaam
MTENDAJI Mkuu wa Wakala ya Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda amesema wamejipanga kuhakikisha wanatoa huduma bora ambazo zitavutia wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi.
OSHA wanashiriki katika maonesho ya biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi wanazofanya kama taasisi.
Akizungumza katika banda la OSHA katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) kwenye viwanja vya Julius Nyerere wilayani Temeke mkoa wa Dar es Salaam,Mwenda amesema katika maonesho hayo mbali na kutoa elimu pia wanatoa huduma ya usajili, kupima afya na kuonesha vifaa wanavyotumia vyenye ubora wa kimataifa, hali ambayo itavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
“OSHA tumeshiriki kwenye maonesho haya ya 48, tunaendelea kusajili waajiri, kupima afya kwa zaidi ya watu 300 na kuonesha vifaa vyenye ubora, hali ambayo inavutia wawekezaji,” amesema.
Amesema lengo la OSHA ni kuhakikisha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kukuza uchumi na kuchochea maendeleo inaonekana kwa vitengo.
Aidha, kuhusu mifumo ya OSHA kusomana na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Mwenda amesema hilo lipo kwenye mikakati yao na kwamba siku chache zijazo kila kitu kitakuwa sawa.
Mtendaji mkuu huyo amesema hadi sasa wameweza kusajili sehemu za kazi 45,000, huku takribani sehemu za kazi 40,000 zikisajiliwa kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa upande mwingine Mwenda amesema katika mwaka huu wa 2024/25 OSHA itaongeza kasi ya kusajili na kukagua sehemu za kazi ikiwemo kwenye vyombo vya habari ambavyo ni wadau wa kubwa kwenye jamii.
Awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Deogratius Ndejembi alizitaka taasisi hizo muhimu katika uchumi wa nchi kuhakikisha mifumo inasomana ili kuleta tija.
Waziri Ndejembi amesema OSHA na BRELA zote ni taasisi za Serikali, hivyo katika keleta tija zinapaswa kusomana kwenye mifumo hali ambayo itapunguza mlolongo mrefu kwa wawekezaji.
“Napenda kutumia nafasi hii, kuwaelekeza OSHA kuwa mifumo yao inapaswa kusomana na BRELA, ili kurahisisha wawekezaji lakini pia kuokoa muda,” amesema.
Amesema hakuna haja ya OSHA kufika katika eneo la uwekezaji dakika za mwisho, bali inatakiwa kujua mapemba ili kuleta ufanisi katika kazi.
Ndejembi amesema iwapo taasisi hizi zitafanya kazi kwa pamoja ni wazi mafanikio ambayo Serikali inahitaji hasa katika huduma kwa wawekezaji yatafanikiwa.
Aidha, Waziri Ndejembi amewataka waajiri kujisajili OSHA, ili kuhakikisha wakala huyo anafanya ukaguzi ambao unahitajika kwenye sehemu za kazi na biashara kama sheria inavyotaka.
“Kusema kweli utendaji wa OSHA chini ya Mkurugenzi Khadija Mwenda na wasaidizi wake unaridhisha ndio maana unaona kasi ya usajili imeongezeka, endeleeni kukaza buti,” amesema.
Pia Waziri Ndejembi ameipongeza OSHA kwa kuzingatia weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yake ya kila siku, huku akiitaka isifanye uaskari na kuwa marafiki wa waajiri, hasa kwa kuwekeza kwenye elimu hasa faida ya waajiri kujisajili kwao.
Amesema OSHA imekuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za kijamii na kuchochea ukaaji wa uchumi na kuitaka iongeze nguvu zaidi.