Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WIZARA ya Viwanda na Biashara inatarajia kuzindua Sera ya Taifa ya Biashara ya 2003 toleo la 2023 ambapo pamoja na mambo mengine itasaidia kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kuvutia uwekezaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Waziri wa Viwanda na Biashara Dk.Selemani Jafo amssema uzinduzi wa sera hiyo ambayo ni marejeo ya sera ya mwaka 2003 iliyofanyiwa marekebisho 2023 yenye kauli mbiyu kauli mbiyu isemayo “Ushindani wa Biashara katika kuchochea Kasi ya Mabadiliko ya Kijamii na Kiuchumi yanayoongozwa na Viwanda” unatarajiwa kufanywa na Naibu Waziri Mkuuu Dk.Dotto Biteko jijini Dar es Salaam Julai 30.
Amesema marekebisho ya sera hiyo yamefanyika ili kuendana na maboresho kwa lengo kukabiliana na mabadiliko yaliyotokea kikanda na kimataifa.
Amesema sera hiyo inatarajia kuleta faida mbalimbali zikiwemo kuongezeka kwa mchango wa sekta ya biashara katika Pato la Taifa,kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara nchini na kuvutia uwekezaji.
“Sera pia itasaidia kuongezeka kwa shughuli za biashara na ajira na kuongezeka kwa kipato cha wananchi,”amesema Dk.Jafo.
Amesema sera pia itasaidia kuimarika kwa uzalishaji viwandani kutokana na upatikanaji wa masoko ya uhakika na hivyo kuchochea jitihada za ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Ameongeza maboresho hayo pia yatasaidia kuwepo kwa ushindani huru na haki katika biashara na kumlinda mlaji na kuimarika kwa uratibu wa biashara na kuondokana na mgongano wa kisera,kisheria na mgawanyo wa majukumu ya kitaasisi katika masuala ya biashara.
“Uboreshaji wa sera hiyo pia utasaidia kuimarika kwa miundombinu ya masoko na biashara,kuimarika na kuongozeka kwa biashara ya nje na kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji wa shughuli za biashara kupitia matumizi ya mifumo ya kibiashara,”amesema Dk.Jafo.
Akizungumzia kuhusu maboresho hayo Dk.Jafo amesema katika mapitio ya sera ya mwaka 2003 yaliyofanywa na wizara ambayo yamesababisha kuja na toleo la 2023 ni maeneo ya kisera yaliyokuwepo awali na kupanuliwa wigo wake na kuongeza maeneo mapya.
Amesema kutokana na hayo sera imejumuisha na kuzingatia malengo mbalimbali ikiwemo kuoanisha sera na kanuni za Biashara na Sera zinazohusiana na masuala ya kibiashara.
“Sera pia imeondoa mgongano wa kisera, kisheria na mgawanyo wa majukumu ya kitaasisi ili kuleta ufanisi katika biashara,kuimarisha, kukuza na kuendeleza biashara ya ndani na nje,”amesema Dk.Jafo.
Amesema pia sera itaimarisha mtangamano na ushiriki wa nchi katika biashara na nchi zingine rafiki, kikanda na kimataifa na kuimarisha uendelezaji na ujenzi wa miundombinu ya masoko na biashara.
Naye Mkurugenzi mkazi wa kampuni ya Trade Mark Afrika Elibariki Shami ameipongeza Tanzania kwakufanya maboresho hayo na kusisitiza kuwa ni vema kila Taifa lichukue hatua hizo za haraka ili biashara ziweze kufanyika kwa urahisi.
“Sera hii itarahisisha kufanya biashara katika maeneo mbalimbali ya kikanda kwa sababu nchi nyingi za Afrika zinashindwa kufanya biashara kwa pamoja kwa sababu ya kukinzana katika sera za biashara,”amesema Shami.