Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imesema inatarajia kuwafikia wateja wapya 250,000 ifikapo Desemba mwaka huu kupitia huduma yao ya ‘TCB Popote’ ambayo itawawezesha wananchi kufungua akaunti kidigitali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Julai 30,Mkuu wa Kitengo cha Ufumbuzi wa Kigitali wa TCB Jesse Jackson amesema lengo la akaunti hiyo ni kuwasogezea wananchi huduma zakifedha karibu.
“Malengo yetu kwakipindi cha miezi minne iliyobaki tunataka kuwafikia wateja laki mbili na nusu ambao watafungua akaunti hizi zakidigitali kupitia simu janja zao,malengo ya mbele zaidi ambayo yataanzia mwakani ambapo tutakuwa tumeshaweka maandalizi kwa ajili ya simu za kawaida tunatarajia kufikia wateja wengi zaidi,”amesema Jackson.
Amesema huduma hiyo ni mwendelezo wa ubunifu unaofanywa na benki hiyo kwakuwa kwa miaka kadhaa TCB imekuwa ikifanya bunifu ili kuleta huduma karibu na wateja.
Amesema lengo lao ni kuwaleta wateja karibu kwakuwa wao ni benki ya tatu kwa matawi na mpaka sasa wana mawakala 6000 Tanzania nzima.
“Tumeona hiyo haitoshi tunahitaji kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi kwakuwa takwimu zinaonesha asilinia 89 ya watanzania wanaweza kupata huduma za kifedha ndani ya kilomita tano na asilimia 22 tu ya Watanzania wana akaunti zakibenki,”amesema Jackson.
“Huduma hii ya ‘TCB Popote’ inafanya mtu anaweza kufungua akunti popote alipo anachohitaji ni simu janja yake na kitambulisho,
akaunti hii ikikamilika itaweza kutoa huduma ya kulipia bidhaa mbalimbali na huduma za mikopo,”amesema.
Awali Mkurugenzi wa Masoko Ukuzaji wa Biashara na Mahusiano ya Umma, Deo Kwiyukwa amesema huduma ya uzinduzi huo ni muendelezo wa bunifu ambapo miezi michache iliyopita walizindua huduma Toboa na Kikoba ambayo wamejiunga na kampuni za simu kuunganisha wateja kwenye vikoba.
“Kwa sasa tumeongeza huduma yakufungu akaunti kidigitali mteja yoyote atakayetaka kuwa na akaunti na na sisi na kupata huduma zetu ataweza kufungua akaunti kidigitali ambayo atapata hudumq zote ikiwemo kulipia bili mbalimbali popote,”amesema Kwiyukwa.