Na Nora Damian, Dodoma
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka wananchi kuongeza umakini katika matumizi ya simu za mkononi na mtandao wa intaneti na kutofungua au kutosambaza viunganishi (links) wasivyovijua kwani vinaweza kuwaletea athari.
Akizungumza jana na Waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji yanayofanyika kitaifa jijini Dodoma, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Umma wa TCRA, Rolf Kibaja, alisema baadhi ya watu wamekuwa si waaminifu wanaweza kutumia njia hiyo kupata taarifa ambazo zinaweza kuleta athari kwa muhusika.
“Katika maonesho haya tumetoa elimu kwa wakulima na wadau mbalimbali jinsi ya kujilinda kutokana na changamoto mbalimbali za mtandao, tumewataka wahakikishe hawafungui link wasizozifahamu. Inaweza kuwa kwenye WhatsApp mtu amekutumia link au kiunganishi kwamba shiriki bahati nasibu au sambaza utapata zawadi fulani, usifanye hivyo…link usiyoifahamu usifungue na wala usisambaze,” alisema Kibaja.
Aliwataka wananchi kuendelea kuhakiki namba zao za simu kwa sababu suala hilo ni endelevu na kuripoti kwa watoa huduma namba wasizozifahamu ili ziweze kuondolewa.
“Wananchi wasipokee maelekezo yoyote kwa mtu anayejifanya kwamba ni mtoa huduma, hakikisha mtu ambaye anakupigia na kukupa maelekezo kwamba ni mtoa huduma anatumia namba 100, tofauti na namba 100 usipokee maelekezo.
“Ni rahisi mtu kutumia namba ya kawaida kumpigia mtumiaji wa huduma za mawasiliano kutaka kuomba taarifa zako au kukuambia kwamba umeshinda bahati nasibu,” alisema.
Alisema katika maonesho hayo wamekutana na wadau mbalimbali ambao wamepewa miongozo ya kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na mamlaka hiyo ambazo mtu anaweza kuhudumiwa kokote aliko kwa kutumia mifumo ya kielektroniki ambayo ni rahisi.
“Mamlaka imeshiriki kwenye maonesho haya ili kuendelea kutoa elimu kwa umma, eneo ambalo watu wengi wamekuwa wakiuliza sana ni jinsi gani ya kuweza kujilinda, kuripoti kama wametapeliwa au kutoa taarifa. Mawasiliano ni muhimu katika uchumi wa kidijiti, ni sekta wezeshi hivyo kuwepo kwetu wakulima wanarahishiwa kwa sababu wanapokuwa na intaneti wanapata taarifa mbalimbali za mazao, simu zinawarahishia kutuma miamala, kununua, kuuza na kuhifadhi fedha,” alisema Kibaja.