Na Nora Damian, Dodoma
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nelson Mlali amesema changamoto zote walizopokea kutoka wadau kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Nanenane yanayoendelea kitaifa jijini Dodoma watahakikisha zinapatiwa ufumbuzi ili kuufanya usafiri wa njia ya maji uwe salama na gharama nafuu.
Akizungumza na Waandishi wa habari alisema changamoto walizopokea katika maonesho hayo zinahusu viwango mbalimbali vya tozo katika mnyororo mzima wa usafirishaji mizigo kwa njia ya bahari huku nyingine zikiwa ni kuchelewa kwa meli kupata gati na kusababisha kukaa bandarini kwa muda mrefu.
“Tulitaka tujifunze changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau wetu wanaotumia usafiri wa maji ili tuweze kuzitafutia suluhisho tukishirikiana na wadau wengine, zinaweza zikawa za kiutalawa au kiutendaji kazi lakini zipo ambazo tunafahamu huenda zitahitaji mabadiliko ya sheria.
“Kwahiyo tunazikusanya ili tukazifanyie kazi baada ya maonesho haya ili kuufanya usafiri wa njia ya maji uweze kuwa salama na gharama nafuu, Watanzania wanapoiona TASAC ipo wajongee ili waweze kupata elimu na suluhisho la changamoto wanazozipata wanapotumia usafiri wa maji.
“Tunaomba ushirikiano hasa kwa wale walio karibu na maji wawe mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba maziwa, bahari au fukwe zetu zinakuwa salama ili kudumisha usafiri kwa njia ya maji,” alisema Mlali.
Alisema TASAC ina uhusiano mkubwa na sekta ya kilimo kwa sababu wao ndiyo wanaosimamia usafirishaji mazao ya kilimo na kwamba zaidi ya asilimia 90 ya mizigo inayosafirishwa inatumia njia ya maji.
“Tunasimamia sekta ya usafiri kwa njia ya maji, tunashughulika na meli na mizigo na kilimo kinatumika kwa ajili ya chakula na biashara, tunasafirisha mazao ya kilimo kama vile kakao, tumbaku, chai, zabibu na mengine kwahiyo sisi tunahusika kwa kiasi kikubwa katika maonesho haya,” alisema.
“Wavuvi wanatumia vyombo mbalimbali, tunadhibiti vyombo vyao kwa maana ya usalama, tunavikagua na kuvipa leseni, pembejeo nyingi na viuatilifu vinaagizwa kutoka nje ambapo huja kwa njia ya maji hivyo tunahusika kwa kiasi kikubwa katika sekta hii,” alisema Mlali.
Alisema pia katika sekta ya mifugo na uvuvi wanahusika kwa sababu wanasimamia watu wanaosafirisha wanyama hai kwenda nchi mbalimbali kama vile Comoro kwa kutumia usafiri wa maji hivyo wanahusika kukagua meli kuhakikisha usafiri huo ni salama wakati wote.