WAGONJWA WA KIHARUSI WAFANYIWA UPASUAJI BILA KUFUNGUA FUVU 

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

TAASISI ya tiba ya mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa mara imefanya upasuaji wagonjwa 11 wenye kiharusi na magonjwa mengine ya mishipa ya damu ndani ya ubongo bila kufungua fuvu kupitia mtambo wa kisasa wa Angio suite (Cath lab) uliopo MOI.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MOI Dkt. Lemeri Mchome amebainisha hayo leo Agosti 14, 2024 MOI alipokutana na kufanya mazungumzo na madaktari bingwa na wabobezi kutoka Taasisi mbalimbali nchini Marekani.

“Leo ni siku ya 5 tangu tumeanza na kambi hii ya uchunguzi na tiba kwa wagonjwa wenye kiharusi MOI ambapo kwa mara ya kwanza wagonjwa 11 wameshafanyiwa upasuaji huo mpaka sasa na hadi kufikia tarehe 17 jumla ya wagonjwa 15 watafanyiwa upasuaji huo” amesema Dkt. Lemeri 

Amesema lengo la kambi hiyo ni kutibu magonjwa yasioambukiza (NCDS) kama kiharusi kwani yamekuwa tatizo kubwa katika nchi yetu na sasa  Taasisi ya MOI imeshaanza kutoa tiba hivyo natoa wito kwa wananchi kufanya uchunguzi afya mara kwa mara hasa wenye matatizo ya shinikizo la damu, mafuta ya lehemu(Cholesterol) na ugonjwa wa kisukari.

Pia Dkt. Lemeri ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha huduma za kibobezi hususani za matibabu ya kiharusi zinaendelea kuimarika na kuwafikia wananchi wote.

Kwa upande wake daktari bingwa Mtanzania kutoka Chuo Kikuu cha Utali, Marekani Dkt. Faheem Sheriff amesema sasa amerudi Tanzania kwaajili ya kuwatibu watanzania wenzake wenye magonjwa ya kiharusi na amewaomba wagonjwa kuja hospitali mapema ila kupata matibabu mapema na kwa matokeo bora.

Naye Daktari bingwa wa ubongo wa MOI Dkt. Alpha Kinghomella amesema wagonjwa wote waliopata matibabu ya ugonjwa  huo wanaendelea vizuri ambao kuna wagonjwa walikuwa na kiharusi cha damu kuganda na wengine kiharusi cha damu kupasua mishipa ya damu na kutoka nje kuingia kwenye ubongo.

Daktari bingwa wa ubongo kwa kutumia mionzi kutoka hospitali za jeshi nchini Tanzania Dkt. Ally Qassim amesema kambi hiyo inawapa matibabu ya kiharusi watanzania ambapo ilitakiwa waende nje ya nchi kutibiwa lakini sasa wanatibiwa hapa hapa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *