Na Mwandishi Wetu,Lindi
MKUU wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack ameutaka uongozi wa Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kuhakikisha wanaendeleza eneo walilopewa na mkoa huo kwa kujenga tawi la chuo hicho.
Taleck amaesema hayo ofisini kwake wakati akiongea na uongozi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam(DMI) walipofika ofisini kwake kwa lengo la kuelezea mpango wa kutoa mafunzo ya usalama kwa wavuvi mkoani hapo.
“Mkoa wa Lindi unawavuvi wengi na asili ya watu wa Lindi ni Uvuvi na Kilimo hivyo ni muhimu kwa chuo chenu kujenga tawi hapa, eneo tumewapa na tupo tayari kufanya kazi pamoja nanyi kuhakikisha wavuvi wanapata elimu stahiki ili kukuza uchumi wa Mkoa wa Lindi na taifa letu” amesema Taleck.
Kwa Upande wake Mkuu wa chuo cha DMI Dk.Tumaini Gurumo amasema kuwa lengo la kufika ofisini kwa mkuu wa mkoa huo ni kumwelezea mpango wa chuo hicho kuqnza kujenga kituo cha mafunzo ya usalama katika utafutaji na uchimbaji wa gesi pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uvuvi salama .
“Tunaushukuru sana Uongozi wa Mkoa ukiongozwa na Mkuu wa Mkoa kwa kutupokea mimi na wenzangu pia kwa kutupatia eneo la kujenga tawi la chuo chetu, hivyo tunaendela kukamilisha taratibu mbalimbali za kuanza ujenzi huo” amesema Dk. Tumaini.
Uongozi wa Chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wa chuo Dk. Gurumo wapo mkoani Lindi kwa siku nne wakiendelea kutoa elimu kwa wavuvi na kutembelea shule mabalimbali za mkoa huo kutoa elimu ya fursa za masomo yanayohusu bahari kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ili wajiunge na chuo hicho ambacho makao makuu yake yapo jijini Dar es Salaam.