Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Philip Mpango ameitaka Wizara ya Madini kuhakisha inasimamia vyema uvunaji wa madini ya kimkakati ili nchi iweze kunufaika nayo.
Dk. Mpango ameyasema hayo leo Agosti 22, 2024 Katika eneo la Mpwayungu,Wilaya ya Chamwino-Dodoma wakati akihitimisha ziara ya siku nne ya Mkoa wa Dodoma.
Amesema, Mwenyezi Mungu ametujaalia rasilimali ya madini mkakati yenye mahitaji makubwa sana duniani.
“Simamieni Kuna fursa nyingi upande wa Madini ujenzi hata kutengeneza mbolea, Mkoa wa Dodoma umebarikiwa kuwa na madini haya mkakati kwa uwingi na aina tofauti tofauti,lazima rasilimali hii ikatafsirike katika maendeleo ya wananchi wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla.”amesema.
Aidha, ameiagiza Wizara ya Madini kuhakikisha inaweka mpango mzuri wa usimamizi wa rasilimali hiyo kwa manufaa ya Taifa na kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Akiwasilisha salamu za Wizara,Waziri wa Madini Anthony Mavunde amemuahidi Dkt. Mpango kuyafanyia kazi maelekezo yote na kwa sasa Wizara inakamilisha andiko la mkakati wa usimamizi na uvunaji wa madini hayo ili yalete faida kwa nchi kwa kuchochea uchumi na kuendeleza sekta ya madini.
Mavunde alitumia fursa hiyo kutoa maelekezo kwa Afisa Madini Wakazi(RMOs) kuhakikisha wanasimamia ipasavyo maeneo yenye uchimbaji wa madini mkakati ili manufaa yake yaonekane kwa Taifa.