‘USAHIHI WA UTABIRI UNASAIDIA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZA HALI YA HEWA’

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema ufanisi katika kutabiri kwa usahihi matukio mbalimbali ya hali ya hewa kunasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali za hali mbaya ya hewa ambayo kwa kiasi kikubwa yamesababisha hasara ikiwemo vifo pamoja na upotevu wa mali kwa nchi mbalimbali barani Afrika.

Profesa Mbarawa ameyasema hayo leo katika ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya rada, mafunzo yanayotarajiwa kufanyika kwa siku tano mkoani Mwanza, ambapo jumla ya nchi 12 kutoka eneo la Afrika Mashariki zinatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo, Baadhi ya nchi hizo ni Burundi,Kenya, Uganda, Rwanda, Uganda, na DRC Kongo.

“Kama tunavyojua ukweli ni kuwa shughuli nyingi za wananchi barani Afrika zinategemea sana hali nzuri ya hewa ili kufanikiwa, lakini majanga mengi yaliyosabisha vifo na upotevu wa mali kwa miaka ya hivi karibuni yana muunganiko na hali mbaya ya hewa,” amesema Profesa Mbarawa.

Aidha ameongeza kuwa kuwepo kwa tahadhari za mapema zinazotokana na ufanisi katika taaluma ya utabiri wa hali ya hewa kutasaidia kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa, kwani itasaidia mamlaka husika na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari kabla ya hatari.

Pia Tanzania ina jumla ya rada tano za hali ya hewa pia rada mbili zinaendelea kutengenezwa nchini marekani zikikamilika zinategemewa kufungwa mikoa ya Dodoma na Kilimanjaro.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk.Ladislaus Chang’a amesema katika kikao cha wakuu wa mamlaka za hali ya hewa Afrika mashariki kilichofanyika nchini Uganda moja ya maazimio yaliyofikiwa ni pamoja na kuiomba TMA kushirikisha uzoefu wake kwa nchi za Afrika Mashariki juu ya namna ya kutumia rada kwa ufanisi katika utabiri wa hali ya hewa.

Muwakilishi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambao ni waandaaji wa mafunzo hayo Dr.Eunjin Choi amesema mafunzo hayo ni muendelezo wa jitihada za shirika hilo kushirikiana na wanachama wake katika kutoa elimu pamoja na mafunzo yenye lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa tahadhari za mapema kuhusu changamoto za hali ya hewa.

Dr. Choi amesema uzoefu kutoka kwa wataalamu mbalimbali katika mafunzo hayo kutasaidia washiriki wa mafunzo hayo kuongeza ufanisi na kuboresha uwezo wa utoaji taarifa kwa usahihi katika mamlaka za hali ya hewa kwenye nchi wanazo toka.

Mafunzo hayo yanayofanyika mkoani Mwanza yameandaliwa  na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)na kuratibiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ambapo yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 30 2024.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *