Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
CHUO cha Bahari Dar es Salaam
(DMI) kimesaini mkataba wa makubaliano na Shirika la Kitaifa la Masuala ya Bahari la Muumgano wa Comoro (NAM) katika masuala ya bahari kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kukuza uchumi wa sekta hiyo.
Akizungumza leo Septemba 3,wakati wakusaini makubaliano hayo Mkuu wa Chuo Cha DMI Dk.Tumaini Gurumo amesema ushirikiano wa Tanzania na Comoro katika masuala mbalimbali yakibiashara umeanza muda mrefu na kwanba katika upande wa masuala ya bahari wameamua kuingia makubaliano hayo maalum kwa lengo la kubadilishana uzoefu hasa katika masuala ya utoaji wa elimu ya bahari.
“Watanzania wengi wapo Comoro wanafanya biashara na Wacomoro wapo Tanzania wanafanya pia biashara,makubaliano haya tunayosaini lengo ni kuhakikisha tunakuwa karibu katika kujenga rasilimali watu za nchi hizi katika masuala ya bahari,”amesema Dk.Gurumo.
Amesema Comoro ni nchi ambayp imeizidi Tanzania katika masuala ya bahari kwakuwa wao wana eneo kubwa lililozungukwa na bahari.
“Wenzetu sio wengi lakini wamezungukwa na maji eneo lao kubwa ni bahari, matumizi ya maji yanahitaji watu wenye weledi,pia kuna masuala ya usimamizi wa meli zilizosajiliwa ni matamani yetu kuwa tutaweza kubadilushana mawazo na kuona wenzetu wakifanya matumizi ya maji kwa ufanisi.
“Tunakwenda kushirikiana kuhakikisha tunapata rasilimali watu yenye weledi kupitia chuo hichi na tutahakikisha chuo chetu kinatoa watu wenye weledi,tutashirukiana katika kufanya research(utafiti) na kujua jinsi gani tunaondoa changamoto zilizopo kwenye sekta ya bahari katika nchi hizi mbili,”amesema Dk.Gurumo.
Amesema kwenye upande wa usajili wa meli Comoro wapo vizuri hivyo DMI wapo tayari kufanya kazi na NAM lengo ni kuhakikisha sekta ya bahari inakwenda kuimarika katika nchi hizo mbili pamoja na za Afrika ambapo mkakato ni kuhakikisha matumizi ya bahari yanaenda sawa.
Naye Mkurugenzi wa NAM ,Mohamed Dahalani amesema asilimia 80 ya wafanyabiashara kutoa Comoro wanakuja Tanzania kuchukua mzigo hivyo ushirikiano wa nchi hizo mbili ni mkubwa.
“Wacomoro mbali na biashara pia tunakuja Tanzania kusoma mambo ya meli na watu wakitoka hapa wanafanya kazi,tunaona Tanzania ipo mbele sana kuliko Comoro kuhusu mafunzo ya baharini tumeona tuje tushirikiane,wanafunzi waliosomea DMI wakija Comoro kule ndo wanashika mamlaka,wengine wapo bandarini wamesomea hapa hapa DMI tumejua watanzania wapo mbele tumeona na sisi twemde mbele zaidi.
“Lakini na sisi tupo mbele zaidi ya kwao sisi kwenye upande wa kusajili meli tupo mbele kwa sababu tulianza zamani haya mambo huku hayapo,kwenye elimu tatizo Wacomoro wengi hawapendi mambo ya bahari sasa tunataka kutumia nafasi hii kuwashawishi ili waweze kujifunza mambo haya ,”amesema Dahalani.