DCEA yakamata kilogramu 1,815 za skanka

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

MAMLAKA  ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imekamata kilogramu  1,815 za dawa za kulevya aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Ukamataji huo uliohusisha watuhumiwa watano wanaodaiwa kuhusika na dawa hizo umefanyika kupitia operesheni  iliyofanyika Agosti 28 hadi Septemba 2 mwaka huu katika maeneo ya Luguruni Mbezi na Magomeni jijini Dar es Salaam 

Akizungumza na waandishi wa habari leo  Septemba 10,jijini  Dar es Salaam Kamisha Jenerali wa DCEA  Aretas Lyimo amesema watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na  Richard  Mwanri (47) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde wilaya ya Kinondon jini Dar es Salaam na Felista  Mwanri (70) mkulima na mkazi wa Luguluni Mbezi wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa hizo za kulevya.

Amesema watuhumiwa  wengine waliokamatwa ni Athumani Mohamed (58) ambaye mfanyabiashara na mkazi wa Tanga, Omary Mohamed (32) dereva bajaji na mkazi wa Buza jijini Dar es Salaam na Juma Abdallah Chapa (36) mkazi wa Kiwalani jijini  Dar es Salaam. 

“Katika opereshen hiyo, gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za usajili T 551 CAB na bajaji yenye namba za usajili MC 844 CZV vilikamatwa,”amesema Kamishna Lyimo.

Kwa mujibu wa Kamishna Lyimo mtuhumiwa Richard Mwanri ni mhalifu ambaye amekuwa akipokea dawa za kulevya kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kisha kuzisambazwa kwa wauzaji wengine katika maeneo mbalimbali nchini. 

Amesema mamlaka imekuwa ikifanya operesheni mbalimbali kwa ajili ya kukamata skanka kutokana na dawa hiyo ya kulevya kuwa na madhara makubwa kwa binadamu .

“Kwa siku za hivi karibuni, dawa za kulevya aina ya skanka zimekuwa zikikamatwa mara kwa mara chini,skanka  ni aina ya bangi ya iliyosindikwa  yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo,figo na ini,”amesema Kamishna Lyimo.

Amesema pia matumizi  ya skanka kwa wajawazito yanaweza kusababisha madhara  kwa mtoto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *