HESLB  KUSHIRIKIANA NA TAASISI TATU KUWASAKA WADAIWA SUGU

Na Aziza Masoud.Dar es Salaam  

BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa kushirikiana na taasisi tatu za kimkakati zimeungana pamoja  lengo likiwa kubadilishana taarifa ili kuwatafuta wanufaika wa mikopo hiyo ambao hawafanyi marejesho.

Taasisi walizoingia nazo ni Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), CREDITINFO Tanzania Ltd ambayo ni taasisi ya uchakataji wa taarifa za waombaji mikopo katika taasisi za fedha.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia alisema lengo la ushirikiano na taasisi hizo ni kuongeza kasi ya kuwasaka wadaiwa wa mikopo ya elimu ya juu hususan waliopo katika sekta binafsi na isiyo rasmi kwa kutumia kanzidata na mifumo ya TEHAMA iliyounganishwa.

Alisema kushirikiana huko  ni utekelezaji wa agizo la  Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ifikapo Desemba mwaka huu kuhusu kusomana kwa taasisi za serikali.

“Katika kazi yetu ya kukusanya fedha za mikopo, tunawahitaji wadau hawa … hivyo tunaomba mtufikishie ujumbe kwa wateja wetu kuwa sasa tunakwenda kufanya kazi na wadau watatu, na wengine tutawatangazia siku chache zijazo … tunalenga kuwafikia wadaiwa wote kwa kutumia mifumo,” alisema Dkt. Kiwia.

Alisema wataendelea kushirikiana  na wadau mbalimbali  na kuboresha  utendaji kazi  wao.

Naye Mtendaji Mkuu wa RITA, Frank Kanyusi  alisema kushirikiana na HESLB  ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa wakati na wametengeneza mfumo taasisi hizo kupeana taarifa  za wanufaika. 

Naye  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Deusdedit Buberwa aliahidi kutekeleza makubaliano hayo na alifafanua kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuhakikisha taasisi za Serikali zinaunganisha mifumo yao ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa CREDITINFO, Edwin Urasa alishukuru kwa taasisi yake kushirikishwa na kutoa wito kwa wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kujitokeza na kuanza kurejesha ili kujijengea uaminifu wa kukopesheka na taasisi za fedha.

“Hili ni jambo jema kama mteja ni mlipaji mzuri, lakini kama si mlipaji mzuri ni vema ukaanza kulipa madeni yako ukiwemo mkopo wa elimu ya juu kwa sababu sisi tuna taarifa za wakopaji kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo HESLB, tunafanya kazi kwa kuzingatia sheria,” alisema Urasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *