Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Imeelezwa kwamba Wizara ya Madini kupitia Mpango wa Uchimbaji Madini wa Kesho yenye matumaini (MBT) kwa vijana watakaohitimu katika Kituo cha Jimolojia Tanzania (TGC) kuwawezesha kwa kuwapatia vifaa na mashine za Uchongaji, Ukataji na Usafishaji madini ghafi zitakazo pelekea kuwa bidhaa bora zenye thamani ya juu.
Hayo yameelezwa Oktoba 16, 2024 na Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde wakati akitoa ufafanuzi kuhusu hoja zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema kuwa, Kituo cha TGC kinatoa mafunzo kupitia vifaa vya kisasa hususan katika uongezaji thamani madini ya vito kwa Ukataji Uchongaji na Usafishaji, hivyo kwa Mwaka wa Fedha wa 2024/2025 wizara kupitia TGC chini ya Mpango wa MBT itawapatia vifaa na mashine za kisasa kwa wahitimu watakaomaliza masomo ili waweze kujiendeleza baada ya masomo kumalizika.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa, lengo la wizara ni kuwa na KanziData inayoonesha maendeleo ya wahitimu katika kuendeleza ujuzi wa kiufundi na ubunifu walioupata na kuutumia katika viwanda vya kuongeza thamani madini nchini.
Sambamba na hapo, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Mpango mwingine ni kuwepo kwa madini mengi ya vito yaliyoongezewa thamani katika ubora mzuri wa muonekano, ukataji, rangi na uzito ambayo yatawekwa katika vituo vya biashara ili kutanua masoko ya ndani ya nchi.
Kwa upande wake , Naibu Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ameeleza kwamba , faida za Mpango wa MBT kwa wahitimu wa TGC ni pamoja na kuwapatia fursa za masoko, kupata ujuzi wa kisasa kupitia vifaa, kukuza ujasiriamali na Kuchangia Maendeleo ya Sekta ya Madini kwa kuongeza thamani madini kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Awali , akiwasilisha taarifa kuhusu Utendaji Kazi wa Kituo cha TGC , Kaimu Mkuu wa Kituo Mhandisi Ally Maganga amesema kuwa, katika kipindi cha Oktoba 2023 mpaka Septemba 2024 jumla ya vipande vya madini ya vito 395 yenye jumla ya uzito wa carat 335.43 yalikatwa
.
Aidha, jumla ya bidhaa 78 za urembo zilitengenezwa kwa kutumia metali za thamani ikiwemo dhahabu na fedha ambapo vinyago vya thamani madini 541 vilitengenezwa.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti , Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Mhe.Kilumbe Ng’enda ameipongeza Wizara ya Madini na taasisi zake kwa kuratibu na kusimamia mipango mbalimbali inayopangwa ndani ya wizara kwa lengo la utekelezaji na kutoa matokeo chanya kwa sekta na taifa kwa ujumla.
Kituo cha TGC kilianzishwa Mwaka 2003 , kabla ya hapo kituo kilijulikana kama Arusha Gemstone Carving Center (AGCC).