Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Anga nchini (TCAA) imesema ipo mbioni kukipa leseni Chuo Cha Usafirisha nchini (NIT) kwakuwa hatua ya mwisho ya ukaguzi ili kukidhi vigezo vya kutoa mafunzo ya urubani nchini.
Akizungumza katika mkutano wa pili wa kimataifa wa lojistiki na Uchukuzi Mkurugenzi Mkuu wa TCAA Salim Msangi amesema chuo hicho ambacho kimeshanunuliwa ndege mbili za mafunzo ya urubani kinaendelea na utaratibu wa kawaida ambapo ili kupata leseni yakutoa mafunzo ya anga nchini lazima muhusika apitie hatua tano za ukaguzi ambapo anakaguliwa kuona kama amekidhi vigezo vya kimataifa vya kufanya shughuli hiyo.
“Chuo kinapaswa kikidhi vigezo vyote ili hata rubani wanayemtoa pale akidhi vigezo vya kimataifa vya kurusha ndege,ndege haina sehemu yakusimaia angani hivyo kulingana na ukaguzi wetu NIT wameshakaguliwa hatua nne na kwa sasa imebaki hatua moja ambayo wakikidhi tutawapa cheti cha kuanza kutoa mafunzo hayo,”amesema Msangi.
Amesema baada ya kuwakagua na kujiridhisha watawapa cheti na leseni ya mafunzo ya marubani ambao watakidhi vigezo vya kimataifa na kuondoa tatizo la uhaba wa marubani nchini.
Akizungumzia kuhusu TCAA amesema taasisi hiyo ina mamlaka ya kusimamia udhibiti na sheria zilizopo katika sekta ya usafiri wa anga nchini na kutoa mafunzo ya kozi fupi.
“Pamoja na NIT kutoa mafunzo ya usafri wa anga na sisi pia tuna chuo chetu kinachotoa kozi fupi fupi ambazo zinafuata mitaala ya usafiri wa anga duniani NIT inatoa kozi ndefu,”amesema Msangi.
Amesema TCAA pia inatoa huduma za uongozaji ndege zote zinaingia nchini ambapo kutokana na uwezo wao na uwepo wa vifaa vya kisasa pia wanasimamia anga la Burundi.
“Burundi kwakuwa nchi hiyo haina vifaa vilivyothibitishwa vya kusimamia anga kwa maana shirika la anga duniani limekasimu mamlaka hiyo kwetu,ndege zote zinazoingia kutoka Burundi tunazimamia ,”amesema Msangi.
Ameongeza kuwa pia wanasimamia viwanja vya ndege na mashirika yaliyopo nchini pamoja na kutoa leseni za urubani wa ndege nyuki(drone) na kuzioa usajili.