Na Mwandishi Wetu,Morogoro
MSIMAMIZI wa uchaguzi katika jimbo la Malinyi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi Khamis Katimba amevishukuru vyama vya siasa kwa ushirikiano mkubwa wanaompatia katika kipindi ambacho nchi inaelekea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na kuongeza kuwa ushirikiano huo umemwezesha kutekeleza majukumu kwa ufanisi.
Katimba meyasema hayo Otoba 5, 2024 katika Kikao cha nne baina yake na Vyama vya siasa Wilayani Malinyi ambapo pamoja na vikao vingine vitatu vilivyotangulia vimefanyika kwa lengo la kutathimini zoezi la uandikishaji na utekeleazaji wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uchaguzi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 2024.
Lengo ni kuhakikisha Malinyi inabaki kuwa salama kuanzia mwanzo wa uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Uchaguzi utapita lakini Wanamalinyi tutabaki,hatuna sababu ya kuwa na vurugu kwa sababu ya uchaguzi, hatuna sababu ya kuwa na uchaguzi utakaotuachia uhasama miongoni mwetu, sisi tunatakiwa tuungane , tuwe kitu kimoja tuendeleze maendeleo,” amesema Katimba
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka uchaguzi ulio imara na uendeshwe kwa kuzingatia 4r zake na mimi kama Msimamizi wa Uchaguzi nazingatia 4r ndiyo maana nimekua nikijibu na kutekeleza kwa haraka na kwa wakati,”amesema Katimba
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Sebastian Waryuba amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo kuwa uchaguzi uwe wa haki kwa kuzingatia 4r, Pia amewashukuru viongozi wa vyama vya siasa kwa kushirikiana na Msimamizi wa uchaguzi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya rufaa ambaye pia ni Katibu Tawala wa Wilaya Saida Mhanga amewahakikishia Viongozi wa vyama vya siasa kuwa atazingatia haki katika rufaa zote na mapingamizi yatakayowasilishwa katika kamati yake.
Sambamba na hilo Mhanga pia amewaomba Viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia kanuni na miongozo ya uchaguzi wakati wa pingamizi kwa kuwa maamuzi yatakayotolewa na kamati yake yatazingatia miongozo hiyo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya Joseph Mwanja amemshukuru Msimamizi wa Uchaguzi kwa ushirikiano na kutenda haki kuanzia katika zoezi la uandikishaji mpaka wakati huu tunapoelekea katika uchaguzi Novemba 27, 2024.
Naye Katibu wa Chama Cha Wananchi (CUF) wilaya Miraji Ngapulila amesema matarajio yake ni kuona hali ya utulivu na uadilifu ikiendelea kuwepo mpaka mwicho wa uchaguzi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo wilaya Abdu Swedi amesema Serikali ina nia njema katika uchaguzi huu hivyo wasitokee watu wachache katika Ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi wasio waadilifu kuharibu nia njema ya ufanyikajji Uchaguzi huu kwa kuzingatia 4r za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.