Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
KATIBU Mkuu wa Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amewataka wadau kuendelea kutumia bandari kavu ya Kwala kwani bandari hiyo inasaidia kupunguza msongamano wa foleni ya malori pamoja na mizigo katika bandari ya Dar es Salaam.
Kahyarara amesema hayo kwenye kikao cha wadau wa bandari kilichofanyika jijini Dar es salaam na kuwakutanisha taasisi za Jeshi la Polisi Ushoroba wa Kati, TRA, TBS, wadau wa bandari pamoja na Wizara ya Uchukuzi.

“ Tukiendelea kutumia bandari kavu ya Kwala itasidia sana kupunguza sana msongamoano wa malori na mizigo katika bandari yetu ya Dar es Salaam” alisema Kahyarara.
Pia Kahyarara amesema kuwa Wizara ya Uchukuzi itakutana na wadau mbalimbali akiwemo mkuu wa mkoa wa Songwe kujadili na kutafuta ufumbuzi wa Msongamano wa Malori katika Mpaka wa Tunduma.

Kwa upande Mwakilishi wa Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam Kapteni John Peter amesema kuwa meli zimezidi kuongezeka katika Bandari ya Dar es Salaam na kazi ya kupeleka makasha katika Bandari kavu ya kwala inaendelea.
“ Meli kubwa za kubeba Makasha na Kichele zimezidi kuongezeka katika bandari ya Dar es Salaam na meli zote zinahudumiwa kwa wakati na kuondoka “ alisema Kapteni John.

Naye katibu Mkuu wa Ushoroba wa kati Flory Okandju amesema kuwa wataendelea kuisaidia TRC kwa kurabati mabehewa ya Mizigo mpaka sasa zaidi ya Mabehewa ishirini yameshakarabatiwa.
