Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam MCHUNGAJI Richard Hananja amelaani vikali tabia ya baadhi ya viongozi wa dini kutumia majukwaa ya kidini kwa ajili ya kujitafutia umaarufu kupitia matukio ya utekaji au kupotea kwa watu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mchungaji Hananja amesema hakuna dini wala mtu mwenye maadili anayeweza kufurahishwa na matukio ya watu kutekwa au kupotea. Amesisitiza kuwa suluhu ya kweli ya changamoto hizo haiwezi kupatikana kwa maneno ya jukwaani bali kupitia vikao halali vya mazungumzo.

Aidha, amewataka viongozi wa dini kuacha kuishutumu serikali na vyombo vya ulinzi kwa tuhuma zisizo na msingi, akisisitiza kuwa vyombo hivyo vinafanya kazi zao kwa mujibu wa sheria. Ametoa wito kwa Watanzania kuwa na subira na hekima, na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Mchungaji Hananja pia amehoji sababu ya chokochoko kuibuka kila taifa linapokaribia uchaguzi mkuu, akidai kuwa mara nyingi hali hiyo hutumiwa na baadhi ya watu kwa manufaa ya kisiasa. Ametahadharisha kuwa mwenendo huo unaweza kuhatarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika hatua nyingine, Mchungaji Hananja amesisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya pande zinazohusika, akieleza kuwa hata maandiko ya kidini yanahimiza matumizi ya “kiti na meza” kama njia ya kuleta suluhu ya kweli katika jamii.
