SIMBACHAWENE AIPA ‘TANO’ PURA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amepongeza Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),kwa kazi ambazo mamalaka hiyo inazifanya.

Hayo aliyasema jana jijini hapa alipotembelea banda la PURA katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yenye Kaulimbiu isemayo Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidijitali Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.

Alisema kuwa anafurahishwa na kazi kubwa inayoifanya PURA ikiwamo kuendeleza vitalu vilivyopo mpakani Kusini ambavyo bado havijaingizwa sokoni.

Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha usimamizi wa sekta ya gesi asilia na kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Charles Nyangi alieleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha nyaraka ambapo baadae vitalu hivyo vitaingizwa sokoni.

Alisema jukumu kubwa la PURA ni kuhakikisha kuna gesi asilia ya kutosha kwa ajili ya kuweza kuzalisha Nishati ya umeme katika sehemu mbalimbali kwenye usafirishaji wa magari.

Aliongeza kuwa kwa sasa PURA ina vitalu maeneo mapya na kwamba wapo katika maandalizi ya kunadi kwa lengo la kuongeza usalama wa Nishati.

Aidha alifafanua kuwa wanadata za kutosha na kwamba serikali ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha nyaraka.

“Tunapokuwa kwenye maonesho kama haya tunawaelezea wananchi majukumu yetu na shughuli kwa ujumla zinafanyikaje na shughuli zinazotokana na mkondo wa juu wa Petroli,” alisema.

Alisema kuwa Nishati ya gesi asilia imekuwa na mchango mkubwa kwa nchi hasa katika uzalishaji wa umeme kwa sababu kwa kipindi kikubwa uzalishaji wa umeme huo umekuwa ukitokana na nishati ya gesi hiyo.

Alisema kuwa kwa sasa serikali imeweza kuwekeza katika bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambapo matumizi ya gesi asilia imeanza kupungua katika uzalishaji wa umeme.

Mkuu huyo alisema kuwa gesi asilia ni Nishati muhimu ambayo wanatoka elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya majumbani na kwenye gari.

Alisema kwa sasa serikali ipo katika hatua mbalimbali za kuwezesha Nishati hiyo iwafikie wananchi wengi hasa katika matumizi ya gari na maeneo mengine.

“Gesi asilia kwa sasa inatumisa zaidi katika mikoa ya Mtwara,Lindi na Dar es Salaam,kuna jitihada mbalimbali zinafanywa kuhakikisha gesi hii inafika maeneo tofauti tofauti nchini kwa awamu,” alisema.

Nyangi alieleza kuwa uwekezaji huo ni mkubwa hivyo utafanywa kwa awamu kwa kadri serikali itakavyokuwa inawekeza katika gesi hiyo.