TAMWA YALAANI MASHAMBULIZI VIONGOZI WANAWAKE MITANDAONI

Na Aziza Masoud Dar es Salaam 

CHAMA Cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA) kimesema kinalaani vikali aina yoyote ya mashambulizi ya kijinsia dhidi ya wanawake  hasa viongozi wa kisiasa kupitia mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo imetolewa leo Juni 27, 2025,Mwasisi wa TAMWA Halima Sharif katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliokutanisha wanachama wa chama hicho jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafakari mafanikio, changamoto na fursa za chama hiki cha muda mrefu chenye historia ya miaka 39 ya utetezi wa haki za wanawake, watoto na makundi yenye uhitaji maalum.

Alisema mitandao ya kijamii imekuwa jukwaa linalokwamisha jitihada za kuwainua wanawake katika siasa na uongozi hivyo chama hicho kimelaani vikali tabia hiyo.

“Ndiyo mitandao ya kijamii ni hatua ya maendeleo lakini pia imekuwa jukwaa linalokwamisha jitihada za kuwainua wanawake katika siasa za uongozi,”alisema Sharif.

Alisema Tamwa inalaani vikali aina yoyote ya mashambulizi ya kijinsia dhidi ya wanawake hasa viongozi wa kisiasa  kupitia mitandao ya kijamii.

Alisema wanaamini kuwa mwanamke mwanasiasa anapaswa kuhukumiwa kwa hoja na misimamo yake ya kisera siyo kwa sababu ya jinsia yake.

“Kudhalilisha wanawake kwakutumia majukwaa ya kidigital9 ni ukiukwajiwa maadili ya Kitanzania na kikwazo kwa maendeleo ya demokrasia jumuishi.

Alisema TAMWA imekuwa chombo muhimu katika kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia, kuhamasisha uundwaji wa sera na sheria zenye mlengo wa usawa wa kijinsia, na kuwajengea uwezo na kuwezesha maelfu ya wanahabari kufahamu kwa kina masuala ya usawa wa kijinsia.

Alisema ni pamoja na afya ya uzazi, ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi, rushwa ya ngono katika vyombo vya habari, ulinzi na usalama wa kitaaluma, na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kazi zao za kila siku.

Amesema kupitia miradi na kampeni zake, TAMWA imechangia katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, kukuza uwezo wa wanahabati zaidi ya 321 kwa mwaka 2024, kuripoti kwa weledi kuhusu ukatili wa kijinsia, kufanya tafiti 2 za masuala ya kijinsia kwa mwaka 2024, kutambulika na

Wizara ya Habari na Teknolojia ya Mawasiliano kama kiungo muhimu kwenye masuala ya usawa wa kijinsia kwenye vyombo vya Habari, kuhimiza vyombo vya habari kutekeleza sera ya jinsia katika mazingira ya kazi.

Kwa upande wakeMkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Rose Reuben  amesema  TAMWA  pamoja na mafanikio makubwa iliyoyapata bado zipo changamoto zinazoendelea kuathiri harakati za usawa wa kijinsia ikiwemo ya ushiriki mdogo wa wanawake katika siasa na uongozi.

Amesema hiyo ni changamoto ambayo TAMWA na jamii ya watanzania kwa ujumla wanatakiwa kupambana nayo kwa dhati ya mioyo yao kwani uchache wa ushiriki wa wanawake katika siasa unaathiri kwa kiasi kikubwa kufikia malengo ya ushiriki wao katika maamuzi muhimu kwa mustakabali wa Taifa.

“Kama tunavyoona kwa Rais wetu uongozi wake umeonesha kwa vitendo kuwa wanawake wanaweza kuongoza kwa mafanikio kama ilivyo kwa wanaume. Kupitia dhamira yake ya kuendeleza taifa tumeona utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo, marekebisho ya sheria ya vyama vya siasa na mchakato wa maboresho ya sheria uchaguzi ukipiga hatua,” amesema

Zaidi ya wanachama 200 wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) wamekutana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutafakari mafanikio, changamoto na fursa za chama hiki cha muda mrefu chenye historia ya miaka 39 ya utetezi wa haki za wanawake, watoto na makundi yenye uhitaji maalum.