Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inaendelea kuwahamasisha vijana na makundi mbalimbali kuendelea kufika katika vyuo vyao kwa ajili yakupata mafunzo ya kazi za majumbani ili kuongeza ufanisi na kupata soko la nje ya nchi.
Akizungumza leo Julai Mosi, 2030 katika Viwanja vya Maonesho ya 49 ya Biashara Dar es Salaam(DITF) maarufu kama Sabasaba Muwezeshaji wa Mradi huo, Debora Mwageni, ambapo alisema mafunzo yanayotolewa na VETA yanalenga kumsaidia mfanyakazi kuboresha mazingira ya kazi na kufanya kazi kwa weledi zaidi.
“Mafunzo haya pia yatamfanya mfanyakazi za ndani apate mazingira bora ya kazi na kuboresha maslahi zaidi,”alisema Mwageni.
Alisema mradi huo pia unamuwezesha mfanyakazi kupata ajira ya kudumu, pia kulinda afya yake na kuweka salama mazingira ya kazi
“Katika mafunzo hayo wanajifunza uandaaji wa chakula na mapishi, usimamizi wa nyumba, usafi, kufua na kunyoosha nguo na malezi ya watoto na wazee,”alisema.

Pia, kuna mafunzo ya kufanya kazi nje ya nchi kama Dubai, Oman, Denmark, Uingereza, Marekani na Italia.
“Tunawajengea uwezo katika stadi za maisha, afya ya uzazi, namna bora ya kuwahudumia watu wanaoishi nao kwa ukarimu na haki zao za msingi,” alisema.
Alisema mradi huo ulianzishwa Aprili mwaka jana na muitikio ni mkubwa, ambapo wafanyakazi wa ndani wanasaidiwa kujua majukumu, wajibu na haki zao
Alisema mpaka sasa wafanyakazi wa majumbani 700 wamefanya mafunzo na kutunikiwa vyeti na kwa lengo la kupata ujuzi mahususi kwa kazi zao.
