Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAKATI Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikizuia michango ya wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani ndani ya Chama hicho, Jumuiya ya Wazazi ya Chama hicho Wilaya ya Morogoro imeingia ‘mtegoni’ kwa kuchangisha michango kwa kigezo cha zawadi kwa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa Ndugu Ally Hapi.
Wakizungumza kwa sharti la kutotaja majina yao baadhi ya wanachama wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Morogoro, wamedai kuchangishwa kiasi cha Sh 20,000 kutoka kila Kata ili kumuandalia zawadi Happi ambaye alitarajiwa kufanya ziara Mkoani Morogoro.
Kupitia kikao cha Baraza la Jumuiya ya Wazazi wilaya, kilichoitishwa Juni 18 Mwaka huu, katika ukumbi wa Halmashauri, wajumbe hao kutoka kila Kata ambao ni Mwenyekiti, Katibu, Malezi pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu kila mmoja alipewa agizo la kuchanga kiasi Sh 5000 kwa ajili ya zawadi hiyo kupitia Katibu wa Jumuiya wa Wazazi Wilaya Emmanuel Nestory Icon.
“Kikao hicho kilikuwa na agenda kuu moja tu ya kuandaa mapokezi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa ndugu Ally Hapi” amesema mmoja wa watoa taarifa hao.

Kwa mujibu wa watoa taarifa hao, Katibu huyo alijinasibu kuwa michango hiyo ni zawadi kwa Hapi ambaye alitarajiwa kupita Mkoani hapo akielekea Dodoma hivyo jambo lililopaswa kufanywa na wajumbe hao ni kuchanga fedha ili waweze kumpatia zawadi.
“Tuliambiwa tunapaswa kukusanya kiasi Cha Sh 1.5 Milioni kwa ajili ya kuchangia mafuta Katibu Mkuu, hilo ni jambo la kushangaza kwa kuwa tunavyojua yeye ndiye alipaswa kutuchangia sisi ambao ni wachanga, lakini hatuna hakika kama kweli hizo fedha zilimfikia” amesema Mjumbe mwingine
Wamesema wanachohisi Katibu wao huyo anafanya hivyo ili kuwafurahisha viongozi wa ngazi ya juu ya Chama hicho Taifa ili waweze kumlinda kutokana na tabia yake ya maamuzi yake kufanya kila anachojisikia kukifanya.
hata hivyo inaelezwa Katibu huyo ameitisha kikao leo tarehe 1/7/2025 katika ukumbi wa CCM Kata ya Kingo cha wajumbe hao huku ajenda yake ikiwa bado haikajulikana hali ambayo pia inazua sintofahamu kutokana na ukweli kuwa kwa Sasa chama kimezuia vikao vyote ili kupisha mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani.
Aidha wamedai kuwa katika siku za hivi karibuni viongozi wa Chama na Jumuiya zake Wilaya ya Morogoro wamekuwa wakifanya mambo yasiyoendana na maadili na miiko ya chama hicho bila kuchulikuwa hatua yeyote, kitendo kinachowafedhehsha wanachama wake.
Hii inakuja ambapo pia baadhi wa wagombea wa nafasi za udiwani ndani ya Wilaya hiyo wameomba kurejeshewa fedha zao walizochangishwa kwa kigezo cha michango wakati wakichukua fomu za kugombea Udiwani hivi karibuni.
Baadhi ya wagombea hao ambao pia hawakupenda majina yao yaandikwe, walidai kuchangishwa kiasi cha Hadi Sh 250,000 kutoka Sh 50,000 waliyopaswa kulipa kwa ajili ya kuchukua fomu kwa ajili ya kugombea Udiwani.
“Tumejaribu kufuatilia kuona kama fedha zetu za ziada tunaweza kurudishiwa ila hatuoni Dalili hizo na badala yake tunaona wamebadiri utaratibu kwa kuweka fomu mbili moja ya kuchukua fomu na nyingine wameipa jina la michango ya ihali, lengo ni ‘kumtega’ mgombea mwenyewe aone kama analipa au halipi” amesema.
Alisema Chama Taifa kimeagiza watia Nia wote ambao wamechangishwa fedha hizo warudishiwa huku baadhi ya maeneo wakiwa tayari wamerejeshewa ila inashangaza Wagombea waliochukua fomu Wilaya ya Morogoro hadi Sasa bado hawajarejeshewa huku wakikuomba Chama Taifa kuwasaidia.