Na Mwandishi Wetu,Morogoro
WANANCHI WA Kata ya Tungi Katika Manispaa ya Morogoro wamelalamikia kitendo kilichofanywa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Morogoro Abdulaziz Abood cha ‘kuwalaghai’ kwa kuzindua kisima ambacho hakitoi maji tangu alipokizindua.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwa masharti ya kutoandikwa majina yao na vyombo vya habari, wananchi hao wamedai Kisima hicho kilichopo katika Kituo cha Afya Tungi kilizinduliwa na Mbunge huyo Juni 23 Mwaka huu na kwamba kuanzia siku hiyo hakijawahi kutoa maji hadi hivi sasa.
” Alikizindua kisima na kukabidhi Afisa Mtendaji wa Kata, siku hiyo maji ambayo yalijazwa kwenye tanki yalikuwa kama sehemu ya kufanikisha uzinduzi huo, na tukaambiwa kuanzia wakati huo huduma ya maji itakuwa inapatikana wakati wote jambo ambalo siyo la kweli” amesema mmoja wa wananchi hao.
“Katika mazungumzo ya Mbunge huyo wakati wa uzinduzi alisema kisima kitaleta nafuu kubwa kwa watumiaji wa kituo cha Afya pamoja na wenyeji wakazi wa eneo letu, hili jambo la aibu, kulikuwa na sababu gani kufanya uzinduzi wa mradi ambao haujakamilika” ameongeza

Kwa mujibu wa mkazi mwingine wa eneo hilo, Abood aliwahakikishia kupata maji ya uhakika kupitia kisima hicho huku akiwapa angalizo na kuwaonya wenye magari ya kuuza maji kutokwenda kuchota maji katika kisima hicho ambacho hata hivyo nusu lita ya maji kwa sasa hauwezi kupata kutokana na kutokuwa na maji.
“Kilichotushangaza zaidi ni kuona saa chache baada ya ‘Mbunge’ kuondoka eneo la uzinduzi, mabomba ambayo kimsingi yalionekana kuegeshwa kwa muda ili kukamilisha zoezi yaliondolewa hali iliyozua taharuki kwa watu wote ambao tulikuwa tunashuhudia kitendo kile, tunaona hizi Kampeni zake zenye nia ya kutudanganya kupitia vyombo vya habari” amesema
Alisema cha kusikitisha zaidi tangu ulipozinduliwa mradi huo wiki mbili zilizopita hakuna hata koki moja ya maji katika kisima hicho, hali inayoleta picha kuwa mabomba yaliandaliwa kwa ajili ya maonesho wakati wa uzinduzi tu kwa lengo la kuongeza msukumo wa kampeni za Ubunge.
Alisisitiza kuwa kwa sasa ni dhahiri kuwa maisha ya maendeleo ya Morogoro mjini yapo katika hali ya kisiasa zaidi kuliko kizalendo kwani ni sawa na kupewa kitu kwa mkono wa kushoto na kupokonywa kwa mkono wa kulia.
Aidha wamesisitiza kuwa huo ni muendelezo wa vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na ‘Mbunge’ huyo kwani tayari kuna malalamiko mengi kuhusu magari ya wagonjwa ambayo amekuwa akiyakabidhi bila kutoa kadi na baadae magari hayo kupotea katika mazingira ya kutatanisha.
