Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WAAJIRI wametakiwa kuweka mazingira mazuri ya kazi kwa wafanyakazi ili wafanyakazi waweze kufanya kazi na waone fahari kuitumikia kampuni ama taasisi husika
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana katika kikao kazi cha Chama Cha wafanyakazi wa Serikali ,a Mitaa (TALGWU) na waajiri,Afisa Tawala mkuu wa jiji la Dar es Salaam Flora Mgonja alisema waajiri waliopo katika mamlaka mbalimbali wanatakiwa kuwakumbusha maafisa utumishi na wakurugenzi kuhusu kuwafuatilia na kuwafahamu wafanyakazi wao ili wajue jinsi ya kuwasiliana nao na kutatua matatizo yao.

“Maafisa utumishi na wakurugenzi jambo kubwa sana la umuhimu ni kuwafahamu watumishi wetu unaweza ukamuona mtu kila siku anachelewa kazini kumbe ana matatizo ambayo anapaswa kusikilizwa.
“Tunatakiwa kujua ni namna gani tunaweza kuweka mazingira bora ya watu,wapo watumishi ambao wanaamka asubuhi hawatamani kwenda kazini kwa sababu ya maafisa rasilimali watu,wakurugenzi ipo sehemu anaitwa Mungu mtu hii inamfanya mtu achukie kazi,”alisema Mgonja.

Alisema ni muhimu kwa kila ofisi kuweka mazingira mazuri ya kazi ili mtumishi akiamka atamani kufanya kazi na kuja kazi.
“Sehemu ya kazi ni sehemu ambayo mtumishi anatakiwa aifurahie ,wito kwa wafanyakazi kuhakikisha anatimiza wajibu wao,”alisema
Alisema yapo malalamiko pia ya wafanyakazi wanasema mnakaa sana ofisini kuliko kwenda kwenda kwenye vituo vya kazi.

Awali Naibu Katibu Mkuu TALGWU Wandiba Ngocho alisema chama chao ndiyo chama ambacho kinatetea wafanyakazi waliopo chini ya mamlaka ya serikali za mitaa ukiacha walimu kuna kundi kubwa la tunaowatetea.
“Kitu muhimu kinafanywa na chama ni kuwafanya wafanyakazi kuwa karibu sana na wanachama wake,ni utaratibu wetu kama chama tunakutana na wadau hawa kila mwaka mwisho wa siku hii ni kama kioo tunajitathimini kila mwaka.
“Tumefanya hii kila mikoa lakini leo ni zamu ya mkoa wa Dar es Salaam,tunawashukuru waajiri pamoja na changamoto nyingi lakini tuna uhusiano mzuri,”alisema Ngocho.

Alisema chama huwa kina utaratibu wa mazungumzo wanakaa wanaongea na waajiri pia kuna watendaji wa mitaa vijiji unataka wafanye kazi kwakutumia kanuni na utaratibu.
