TANESCO YANOGESHA SABA SABA KWA KUGAWA  ZAWADI  YA MAJIKO YA UMEME

Na Aziza Masoud,Dar es Salaam

SHIRIKA la Umeme nchini (Tanesco) limetoa zawadi ya majiko ya umeme kwa wananci waliofika katika banda lao lililopo katika Viwanja vya Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ambao wamejibu maswali vizuri waliyoulizwa walipotembelea katika banda hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 7,2025 katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji Tanesco, Lazaro Twange  amesema  katika banda la Tanesco kuna majiko hayo ya umeme na wananchi waliojibu vema maswali waliyoulizwa wamepata fursa ya kujishindia zawadi ya majiko hayo kwa ajili ya kuyatumia katika kupikia.

“Haya ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watanzania wanapaswa  kuhama kwenye kutumia nishati isiyokuwa safi za mikaa na kuni na kutumia iliyosafi, hivyo hapa tunazungumzia nishati ya umeme na tuna majiko haya ya umeme yamefanyiwa utafiti na kuthibitika kuwa yanaweza kupikia na chakula kikaiva kwa kutumia chini ya Unit moja,”alisema Twange.

Aliwaita Watanzania kufika katika banda hilo la Tanesco  na kwa kuzingatia kuwa wanaelewa wanawashindanisha kwa maswali, aliyeshinda amepata zawadi ya jiko la Umeme, hivyo wakayatumie hayo majiko na wawe mabalozi wazuri kwa wengine.

Amesema wananchi waliofika katika banda lao wamepata kupata elimu juu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia ili waweze kuachana na matumizi ya nishati isiyo safi.

Kwa upande wa Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Sadock Mugendi amesema wamekuwa wakisambaza na kusafirisha umeme maeneo mbalimbali vijijini na kwamba hivi karibuni wamemaliza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora mjini kuelekea Katavi wenye kilomita 383 na una msongo wa Kilovolt 132.

“Mradi huu ni mafanikio makubwa kwa Serikali hata hivyo tuna mradi mwingine Mbeya, Katavi yote tunasambaza umeme vijijini, tunaishukuru serikali kuendelea kutuamini kwa kutupatia miradi hii,” amesema

Naye Meneja Mkuu Kampuni ya Uendelezaji Joto Ardhi Tanzania (TGDC), Mathew Mwangomba amesema kwa sasa TGDC katika maeneo ya Mbeya wameanza kuhakiki rasilimali ya joto ardhi na kwamba umeme utakaopatikana utaingizwa  moja kwa moja  kwenye Gridi ya Taifa.

“Timu yetu ipo Mbeya eneo ya Mbozi na baada ya kufanya uhakiki tumebaini kuwa eneo hilo lina uwezo wa megawati 70 ambayo tutaingiza katika gridi ya Taifa, TGDC tunawaalika wadau wote wa ndani na nje kuja kuwekeza katika kampuni yetu,” amesema