Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC) Mohamed Salum amewataka vijana kujiunga na vyuo vinavyotoa kozi za masuala ya madini kwakuwa sekta ya Usafiri Majini bado ina uhaba mkubwa wa mabaharia.
Hayo ameyasema jana Julai 7,2025 na Salum wakati alipotembelea banda la TASAC kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DTiF) yanayofanyika katika Viwanja vya Julius Kambarage Nyerere Jijini Dar es Salaam.

Alisema vijana wengi wamekuwa wakisomea sekta zingine ambazo zimekuwa na watu wengi kwenye soko na kuacha Sekta ya Bahari ambayo ina fursa nyingi za ajira na uhitaji mkubwa wa wasomi.
“Wazazi na walezi nawaomba muwahamsishe watoto wenu kusomea sekta ya Bahari ikiwemo ubaharia,hii ni fursa kubwa ambayo mtu akimaliza ana uwezo wa kufanya kazi ndani na nje ya nchi,”alisema Salum.

Alisema TASAC imeshiriki maonyesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara kwa lengo kutoa Elimu juu ya majukumu ya Wakala huu ikiwemo kudhibiti usafiri majini pamoja na kuchagiza sekta ya usafiri Majini.
“Ukitembelea Banda letu utajua fursa zinazopakana ikiwemo mfuko wa mafunzo ya Sekta ya Bahari,pia kwa upande wa wanawake wanapata fursa ya kusomea sekta ya Bahari “amesema Mkurugenzi Mkuu huyo wa TASAC,”alisema.

Alisema kuwa Wakala huo umekua ukisajili vyombo vya majini nakuvipa cheti cha ubora ,kwa ajili ya kufanya shughuli zake majini,ikiwa lengo ni kudhibiti sekta ya usafiri Majini.
Ameongeza kuwa kupitia Wataalamu wake imekua ikifanya ukaguzi wa Meli za kimataifa zinazoingia nchini,pamoja na uwanda mzima wa Bahari ikiwemo kutoa taarifa ya uokoaji,hali ya hewa,na taarifa kwa wavuvi ili kuweza kuchukua tahadhari,nakuhakikisha Bahari inabaki safi.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa TASAC ameendelea kusema kwamba Wakala huo umekua ukisimamia usalama wa bandari,kutoa leseni za bandari, kusimamia shughuli zote za ujenzi wa bandari.
