ACP  MWAKABONGA:TUSAIDIANE KUPUNGUZA AJALI ZA BODABODA

Na Mwandishi wetu,Dar es Salaam

JESHI la Polisi nchini kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani wameishukuru kampuni ya  Oryx  Energy kwakutoa elimu na msaada wa vifaa muhimu vya kiusalama kwa maafisa usafirishaji maarufu kama bodaboda  na kutoa  wito kwa kampuni nyingine kuiga utaratibu huo ili kupunguza ajali za barabarani.

Msaada huo ambao umetolewa kupitia kampeni ya ‘chuma kwa chuma sio Poa’ yenye lengo la kuongeza uelewa kuhusu masuala ya barabarani kwa madereva bodaboda zaidi ya 200 nchini pia imeenda sambamba na kukabidhi vibanda vya kisasa vya askari kujikinga jua barabarani.

Akizungumza leo Julai 19, 2025  baada yakupokea msaada huo  Kamishna Msaidizi wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani ACP Joseph Mwakabonga alisema zoezi la kutoa elimu ya usalama barabarani ni suala mtambuka ambalo kila mtu anatakiwa kushiriki.

“Kutoa elimu ni suala mtambuka ambalo kila mtu anatakiwa kushirik pamoja na kuwapa vifaa maafisa hawa wa usafirishaji,elimu hii italifanya kundi hili waachane na tabia yakutokufuata sheria za barabarani kwakuwa ndiyo msingi wakupunguza ajali barabarani,tunaweza kupunguza vifo kama jamii itashirikiana kuwaelimisha.

“Ajali  za barabarani bado ni changamoto kubwa nchini, hivyo ushiriki wa wadau kama Oryx Energies katika kutoa elimu ya usalama barabarani ni jambo la kupongezwa na hii chachu kwa wadau wengine,”alisema ACP Mwakabonga.

Akizungumzia kuhusu vibanda vitabo vilivyokabidhiwa kwa ajili ya askari wa jiji la Dar es Salaam alisema  vibanda hivyo ni vya kisasa na vitasaidia askari wa kikosi cha usalama barabarani kutekeleza majukumu yao vizuri kwakuwa vimefungwa mfumo wa taa zinazotumia nishati ya jua (solar), hivyo kuwawezesha kufanya kazi hata wakati wa giza.

“Askari polisi sasa wanaweza kutekeleza majukumu yao wakati, kwani vibanda hivi vina taa zinazotumia nishati ya jua. Hii inaongeza ufanisi wa kazi zetu hata nyakati za usiku,” amesema.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Gas Tanzania Ltd, ambayo ni moja ya kampuni zilizo chini ya Oryx Energies, Benoit Araman, amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kuelimisha na kuhamasisha usalama barabarani, hasa kwa waendeshaji wa pikipiki na bajaji ambao ni sehemu muhimu ya usafiri wa kila siku.

“Tumekuja kuzindua kampeni ya chuma kwa chuma hii inawalenga zaidi  waendesha boda boda na bajaji kuwapa elimu ya usalama barabarani ,tumechagua kundi hili kwa sababu watu  wengi wanashughulika na gari.

“Kampeni hii itawapa fursa yakupata elimu ya usalama barabarani pamoja na matumizi sahihi  ya vilainishi,tunaamini kwamba kwa pamoja tunaweza kupunguza ajali, kulinda maisha, kutumia nishati safi na kusaidia katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa letu,”amesema Araman.

Amesema kampuni hiyo pia wameto vibanda vya kujizuia jua polisi ili kurahisisha utendaji wao wa kazi 

Amebainisha kuwa Oryx Energies pia imekuwa mstari wa mbele katika kushirikiana na kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhusu kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Oryx Energies Tanzania,Imani Mtafya, amesema kuwa kampeni hiyo imelenga kuongeza uelewa na kuchochea mabadiliko chanya kwa waendesha pikipiki, bajaji na watoa huduma wengine kuhusu usalama barabarani.

Ameeleza kuwa malengo ya kampeni ya “Chuma kwa Chuma Sio Poa” ni pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa waendeshaji wa Pikipiki na bajaji kupitia ushirikiano na Jeshi la Polisi; pamoja na kutoa michango ya vitendea kazi kama vile vibanda vya kisasa vya askari vinavyotumia nishati ya jua, kofia ngumu, jaketi za kuonekana usiku, vizimia moto na vilainishi bora kwa mitambo, pikipiki na magari.

Aidha, kupitia kampeni hiyo, kampuni hiyo imetoa mafunzo ya usalama kwa wasafirishaji zaidi ya 200 kwa kila Wilaya Mkoa Dar es Salaam, huku ikilenga kutoa mafunzo mikoa yote.

Mtafya ametoa mwito kwa wasafirishaji na watumiaji wa pikipiki kuchangamkia fursa ya mafunzo na kuwa mabalozi wa usalama barabarani katika jamii zao.

“Ajali nyingi zinaweza kuzuilika, elimu na uwajibikaji ni silaha kubwa zaidi,” amesisitiza  Mtafya.

Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Boda Boda na Bajaji Tanzania Saidi Kagomba  aliendelea kusisitizakwakuwataka wadau kutoa elimu ya usalama barabarani kwakuwa tasnia hiyo imekuwa ikipokea watu wapya kila siku.

“Tunashukuru kwa elimu,kofia ngumu (elementi),vizibao na  vilainishi kutengeneza pikipiki zetu,kikubwa ni kutoa elimu kila kwakuwa kila mwaka unavyogeuka tunapokea watu wengi kutoka maeneo mbalimbali wengi wanakuja hawana elimu yakutambua sheria na kanuni za usalama masuala ya barabarani,usipojua ndo tunakuwa na watu wengi  ambao wanasababisha ajali,”alisema Kagomba.

Alisema kila dereva mmoja wa bodaboda anabeba watu zaidi ya 20 kwa siku kwa  hiyo  kutolewa kwa elimu kutafanya kuwepo na usalama zaidi wa abiria.