Na Asha Mwakyonde, Dodoma
SEKTA ya Maliasili na Utalii imeendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuendeleza na
kuhakikisha uhifadhi mzuri wa maliasili sambamba na upatikanaji
endelevu wa huduma za kiuchumi, kijamii na kimazingira kwa
jamii katika serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yaliyasemwa juzi jijini hapa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Mstaafu ,Balozi Simon Sirro, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya Rais Dk.Samia alisema katika kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025, Mkoa huo umefanikiwa kufanya hifadhi endelevu kwa misitu ya Vijiji141, yenye jumla ya hekta 91,691 katika Halmashuri zote za Wilaya.
Alieleza kuwa mafanikio mengine ni usimamizi wa misitu ya halmashauri tatu za Uvinza (Msitu wa Masito na Lyabutongwe) na Kasulu (Msitu wa Makingi)
zenye ukubwa wa hekta 208,556 na uendelezaji wa misitu 13 ya hifadhi ya Serikali Kuu yenye ukubwa wa hekta 222,919 na Usimamizi wa kitalu kimoja cha uwindaji chenye ukubwa wa hekta 100,000 kinachoitwa Makere-Uvinza Open Area Hunting Block.

Balozi S Sirro aliongeza kuwa uendelezaji wa Hifadhi za Nyuki ambapo jumla ya misitu sabaya Vijiji imetengwa na kuwa hifadhi za nyuki katika Wilaya zaKakonko, Kibondo na Kasulu na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imefanikiwa kuingiamkataba wa kuuza hewa ya ukaa katika Msitu wa Masito.
Alisema kuwa kufanyika kwa ugawaji wa ardhi kwa matumizi ya kilimo na ufugaji kwa wananchi, ambapo jumla ya hekta 10,000
zilitolewa kutoka kwenye Msitu wa Makere Kusini na kugawiwa katika Kijiji cha Mvinza hekta 2,174, Kijiji cha Kagerankanda hekta 2,496 na Halmashauri hekta 5,342 kwa ajili ya wakazi wengine kwa shughuli za maendeleo.

“Mafanikio mengine ni kushirikiana na wadau wa mazingira Mkoa umeendeleza kampeni za upandaji miti ambapo kuanzia 2020 hadi kufikia mwaka 2025, jumla ya miti Milioni 34.5
imepandwa katika wilaya zote za Mkoa wa Kigoma. Lengo ni kuongeza uoto wa asili, kuhifadhi vyanzo vya maji, na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi,” alieleza.
Akizungumzia sekta ndogo ya Utalii
alisema katika kipindi cha 2020 hadi 2025, Mkoa wa Kigoma umeendelea kunufaika na uwekezaji wa Serikali katika kukuza utalii, ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya kitalii kama vile Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Hifadhi ya Taifa ya Mahale, Ziwa Tanganyika pamoja na vivutio vya kihistoria na kiutamaduni kama Kituo cha
kumbukumbu ya Dk. Livingstone kilichopo Ujiji.
Balozi Sirro aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mine ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita Watalii wa ndani wameongezeka kutoka 630 mwaka 2020 hadi 11,769 mwaka 2025 ambapo watalii wa nje wameongezeka kutoka 345 mwaka 2020hadi 655 kufikia mwaka 2025.
