Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kimekemea tabia ya baadhi ya madereva wa pikipiki kubeba mizigo hatarishi inayozidi ukubwa wa vyombo vyao kama milango, mageti au makabati kwakuwa inachangia kusababisha ajali za barabarani.
Kauli hiyo ameitoa mwanzoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Usalama Barabarani Chang’ombe, Reverent Nkyami,wakati uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus inayotengenezwa na kampuni ya Karimjee Value Chain Limited.

Alisema ajali nyingi za bodaboda zinatokana na makosa yanayofanywa na madereva ikiwemo kubeba vitu vikubwa vinavyozidi uwezo.
“Bodaboda mnatabia yakubeba kila kitu,unakutana na mtu barabara kabeba kabati,meza ama geti vifaa hivyo so vyakubebwa na pikipiki matoke yake mnasababisha vurugu barabara pamoja na ajali,”alisema Nkyami.
Alisema ili kupunguza ajali za barabarani madereva wa bodaboda wanapaswa kuwa wastaraabu na vitu wanavyobeba pamoja na kufuata sheria za barabarani.

Nkyami pia alionya kuhusu hatari kubwa iliyopo katika maeneo ya kuvukia waenda kwa miguu maarufu kama ‘Zebra crossing’, kuwa yamegeuka chanzo cha ajali badala ya kuwa sehemu salama.
Mbali na hilo pia alitoa wito kwa waendesha pikipiki na magari kusimama wanapofika kwenye zebra ili kutoa nafasi kwa watu kuvuka salama.
Nkyami alitoa tahadhari pia kwa abiria hususani wanawake kuketi upande kwenye pikipiki kwasababu ni hatari endapo pikipiki itashika breki za ghafla abiria anaweka kudondokea kisogo na kupoteza maisha.

Alisema ukosefu wa elimu rasmi na mafunzo ya usalama barabarani umechangia waendeshaji wengi wa pikipiki kuendesha bila kuzingatia sheria, hali inayochochea ongezeko la ajali na vifo barabarani.
“Kumekuwa na tabia ya kujifunza siku mbili tu mitaani, kesho mtu anaingia barabarani bila uelewa wa sheria. Mbaya zaidi anapakia abiria zaidi ya uwezo (‘mishikaki’), hana stadi ya kuendesha kwa usalama na mwisho wa siku anagongwa au anasababisha vifo,” alisema Nkyami.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limeendelea na juhudi za kutoa elimu kwa waendesha vyombo vya moto pamoja na kufanya oparesheni mbalimbali, zenye lengo la kuongeza uelewa kwa madereva na kupunguza ajali barabarani.

“Asilimia kubwa ya ajali zinahusisha pikipiki, iwe ni dhidi ya waenda kwa miguu, magari au hata pikipiki kwa pikipiki. Hivyo tumejikita katika kutoa elimu zaidi kwa bodaboda ili kukomesha hali hiyo,” alibainisha.
Aidha, aliwataka waendesha pikipiki kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo yanayoendeshwa na jeshi hilo ili kuongeza maarifa, weledi na kuwa salama wawapo barabarani.
Mkuu wa Kitengo cha Vilainishi kutoka Kampuni ya Karimjee Value Chain Limited, Anam Mwemutsi, alisema bidhaa hiyo mpya itamaliza tatizo sugu la uchakachuaji wa vilainishi linalosababisha uharibifu wa injini za pikipiki.
“Tumeleta kilainishi chenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 5,000 bila kubadilishwa, tofauti na sasa ambapo wengi hubadilisha kila baada ya wiki moja. Hii itapunguza gharama na kuongeza ufanisi wa vyombo vya usafiri,” alifafanua Mwemutsi.

Awali Msemaji Msaidizi wa Shirikisho la Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Msisiri, aliipongeza kampuni hiyo kwa kubuni suluhisho litakalosaidia kuimarisha usalama wa vyombo vya usafiri na kupunguza ajali zitokanazo na ubovu wa pikipiki.
“Tatizo la vilainishi vilivyochakachuliwa limekuwa likitutesa kwa muda mrefu. Kupatikana kwa bid has hii bora ni hatua kubwa kwa usalama wetu,” alisema Msisiri.
Uzinduzi wa kilainishi kipya cha Caltex Ezy 4T Plus uliambatana na uzinduzi wa kampeni ya usalama barabarani kwa waendesha bodaboda na bajaji.

Kilainishi hicho kimetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na kimekusudiwa kupunguza gharama za matengenezo ya vyombo vya moto hususani pikipiki.
