Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
WADAU watakiwa kushirikiana katika kutoa elimu ya usalama na maendeleo ya kijamii kwa wanafunzi wangali bado vijana ili kuwekeza katika Taifa salama la badae.
Akizungumza katika shule ya sekondari ya Ndalala wakati wa uzinduzi wa mradi wa Via Creative unaosimamiwa na kampuni ya nishati ya Total Energy,Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Temeke Sadath Mtware alisema ni muhimu taasisi zishirikiane katika kutoa elimu ya usalama barabarani.
“Tukishirikiana kuwapatia wanafunzi maarifa ya usalama barabarani sasa angali wakiwa bado vijana wadogo, tutaweza kuwekeza katika Taifa salama la hapo baadaye, na kupata mafanikio makubwa zaidi,”alisema Mtware.

Mtware alizishauri taasisi nyingine binafsi kuiga mfano huo kwa kuwekeza katika elimu ya usalama na maendeleo ya kijamii.Kwa wanafunzi wa Ndalala na wengine kote nchini, ninyi ndiyo sababu ya kuwepo kwa mradi huu.
“Ninyi ndiyo tumaini la kesho tumieni fursa hii kujifunza, kubuni, kushirikiana na kuwa mfano bora wa kutekeleza mnayojifunza Taifa linawaangalia kwa matumaini,”alisema Mtware.
Alisema kama ofisi ina furaha kubwa kusimama mbele kwa ajili ya kushiriki uzinduzi rasmi wa mradi wa VIA Creative kwa mwaka 2025 katika shule ya sekondari Ndalala.
“Napenda kutoa shukrani za dhati kwa TotalEnergies Marketing Tanzania Limited kwa kunialika na kwa kuendelea kuonyesha dhamira ya dhati katika kulinda usalama wa vijana wetu na kuwawezesha kielimu.
Alisema usalama barabarani ndio kaulimbiu iliyokusanyisha watu katika eneo hilo kutokana na hali halisi ya maisha ya kila siku.
Alisema usalama barabarani hauhitaji tu barabara nzuri, bali pia uelewa wa sheria na kanuni za usalama barabarani, tabia sahihi, na uwajibikaji wa pamoja.
“Kila mwaka, maisha ya watu wakiwemo wanafunzi hupotea kutokana na ajali zinazoweza kuzuilika.
“Nimefurahi zaidi kuona wameanza na shule ya Sekondari ya Ndalala iliyopo kwenye wilaya yetu ya Temeke kwani vijana wetu wa sekondari ni watumiaji wakuu wa barabara kwa kutembea, kuendesha baiskeli, na hata baadhi yao kutumia bodaboda ambazo zimekuwa chanzo ya ajali nyingi za barabarani nchini,”alisema Mtware.

Awali Mkurugenzi wa Sheria na Uhusiano wa Kampuni ya Total Energy Tanzania, Getrude Mpangile alisema mradi wa Via Creative ulianzishwa mwaka 2022 kwa ushirikiano na TotalEnergies Foundation na kutekelezwa na NafasiArt Space.
” VIA kama jina la mradi lilivyo inamaanisha “barabara” na jina hili likiwakilisha lengo kuu la mradi huu yani kuhamasisha elimu ya usalama barabarani kwa msisitizo mkubwa juu ya usalama wa barabarani.

“Kuanzia mwaka 2022 hadi 2024, VIA Creative ililenga wanafunzi wa shule za msingi na kufikia zaidi ya wanafunzi 22,000 katika shule 60 zilizopo Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani, na Morogoro,”alisema Mpangile.
Alisema baada yakufanikiwa kwa mradi huo wanapanua lengo zaidi la mradi huo kwa kufikia wanafunzi wa sekondari kwakianza na shule ya Sekondari Ndalala na kuongeza mkoa wa Dodoma.
Alisema programu ya VIA Creative unaotekelezwa na Nafasi Art Space kwa kupitia ujuzi wao wa ubunifu,wanafunzi watafundishwa usalama barabarani si kwa nadharia tu, bali kupitia muziki, maigizo, na sanaa za kuona.
“Mbinu zinazovutia, kujenga kujiamini, na kuamsha uelewa wa muda mrefu. Zaidi ya hayo, wanafunzi watapata fursa ya kushiriki katika shindano la kitaifa, wakionyesha maarifa ya usalama barabarani na ujuzi walioupata,”alisema.
Alisema shule itakayoshinda kitaifa itapata heshima ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kikanda, jambo linaloleta fahari ya kitaifa na pia ushirikiano wa kikanda juu ya maadili ya usalama barabarani.
“Aidha mshindi wa kitaifa wa shindano la VIA Creative watapatiwa utekelezaji wa pendekezo au mapendekezo watakayo toa kwaajili ya uboreshaji wa usalama wa barabarani.

“Hatua ilitekelezwa kwa mara ya kwanzia kwenye tolea la mradi huu mwaka 2024 ambapo shule ya msingi ya Makuburi walipendeeza kujengewa Ukuta wa shule ambao tulishanikiwa kufanikisha na leo hii shule ya msingi ya Makuburi ina Uzio unaowalinda wanafunzi dhidi ya magari na boda boda zilizokuwa zikipita na kuegeshwa kwenye uwanja shule,”alisema.
Alisema mradi huo wa VIA Creative si mradi tu bali ni harakati inayokua inayowawezesha vijana kuwa mabalozi wa mabadiliko kwa ajili ya usalama barabarani.
Alisema kwa kuanzisha elimu ya usalama barabarani mapema, inachangia moja kwa moja kupunguza ajali za barabarani zinazowahusisha wanafunzi. Pia inaendana na kuunga mkono juhudi za serikali na jeshi la polisi wa usalama barabarani katika kupambana na ajali na kukuza utamaduni wa usalama barabarani.

Alisema mradi wa VIA Creative kwa mwaka 2025 inalenga kufikia wanafunzi katika shule saba nchini Tanzania.
Alizitaja shule hizo ambazo ni shule nne za msingi ambazo ni Makuburi, Buza, Ubungo National za jijini Dar es Salaam, na Mnadani ya Dodoma, Shule ya sekondari ya Ndalala.
Alisema pia mradi utaifikia shule mona ya mahitaji maalum ambayo ni shule ya msingi ya Buguruni yenye wanafunzi wenye changamoto ya usikivu watakaopata mafunzo maalum ya usalama barabarani.

Alisema lengo lao ni kuwafikia zaidi ya wanafunzi 7,000 na kukuza mabalozi 110 wa usalama barabarani kupitia mbinu shirikishi zinazotumia sanaa kuhamasisha uelewa na kuleta mabadiliko chanya.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya Sekondari Ndalala Sylvia Majaliwa aliishukuru kampuni ya Total Energy kwakuwapa mradi huo kwakuwa katika eneo hilo zipo shule nyingi
“Tunashukuru sana sana kwakutufikiria kutuletea huu mradi,kupitia mradi huu naamini tutakuwa na mabalozi wazuri wa usalama barabarani, usalama wa wa watoto ni muhimu kwa ajili ya watu wote na jamii,”alisema Majaliwa.
