Na Aziza Masoud,Dar es Salaam
MKURUGENZI wa Kampuni ya MILLEN ,Millen Happiness Magese ameishauri jamii kuachana na fikra potofu kwamba urembo ni uhuni kwakuwa majukwaa hayo yanahamasisha wanawake kujitambua na kujiamini.
Millen ambaye ndiye muandaaji wa shindano la Miss Universe kwa upande wa Tanzania alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wa warembo watakaoshiriki shindano hilo kwa mwaka 2025.

Amesema shindano hilo, lina lengo la kuhamasisha wanawake kujitambua, kujiamini na kutumia majukwaa ya urembo kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
“Tunataka kuleta utofauti na kubadilisha mtizamo hasi kwa jamii kwamba majukwaa la urembo yanaweza kutumika kuleta mabadiliko chanya ya kimaisha kwa wasichana kuonyesha vipaji vyao na kufahamu namna bora ya kuvitumia katika ustawi wa maisha yao na ya wengine,”alisema Magese.

Kwa mujibu wa Millen, jukwaa hilo limejikita katika kumwezesha mtoto wa kike au mwanamke kuanzia umri wa miaka18 bila kujali ameolewa, hajaolewa ana mtoto au laa, mrefu au mfupi, mwembamba au mnene, bali wote watapata fursa kushiriki katika shindano hilo.
“Washiriki watapimwa kwa vigezo mbalimbali ikiwamo ubunifu, ujasiri, mawasiliano, uelewa wa masuala ya kijamii, pamoja na muonekano wa jumla na litakuwa na majaji wa shindano ambao miongoni mwao kuna watu mashuhuri katika sekta ya mitindo, sanaa, mawasiliano na maendeleo ya jamii kutoka ndani na nje ya nchi.

Alisema wanaamini kwamba mwanamke akipewa nafasi anaweza kutimiza ndoto zake, hivyo amewashukuru wazazi kwa kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika shindano hili muhimu ambalo litawapa fursa ya kuonyesha vipaji vyao mbalimbali,”amesema Magese.
Amesema washiriki katika shindano hilo kwa awamu hii wamepatikana katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Dodoma,Mbeya na kwamba, kwa mara ya kwanza katika historia ya urembo wamefanikiwa kupata washiriki kutoka Zanzibar.

“Kipekee niishukuru serikali kwa kunipa nafasi ya kuleta urembo kwa sababu lengo ni kumuwezesha mwanamke na si kumdhalilisha au kumharibia mambo makubwa ya mila na desturi,”amesema Magese.
Alisema shidano hilo litakuwa linaoneshwa kila siku kupitia vipindi vya runinga kuanzia sasa mpaka mwisho wa shindano.

Judith Ngussa ambaye ni Miss Universe Tanzania 2024 ametumia nafasi hiyo kuwashukuru mabinti wote waliojitokeza kwenye maonesho hayo ya Miss Universe katika mikoa yote waliyopita.
“Tunawashukuru wazazi kwa kuwaruhusu mabinti zao lakini na wao wenyewe kwa juhudi zao na kuiamini kampuni ya dada yetu Millen ambaye amewekeza kwa ajili ya kuwawezesha mabinti wa Tanzania kupitia Jukwaa hili la Miss Universe.Hivyo naiomba Serikali kujitokeza na kutuunga mkono katika uwekezaji wa Miss Universe.”


