Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imewataka wawakilishi wa taasisi na asasi za kiraia kuhakikisha wanatoa mawazo ambayo yatasaidia kuepusha dosari ambazo zinaweza kujitokeza na kuathiri utekelezaji wa shughuli za uchaguzi.
Akizungumza leo Julai 30, 2025 wakati wa kufungua kikao cha wadau hao,Mwenyekiti wa INEC Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele alisema tume inawatambua wawakilishi na taasisi za asasi za kiraia kwa namna mbalimbali kwakuwa ni daraja linalounganisha tume na wadau kwa njia ya elimu pia ni mojawapo ya wadau muhimu.

“Kikao hiki kinatoa nafasi ya kubadilishana na kupeana uzoefu wa utekelezaji wa shughuli za uchaguzi ili kuhakikisha tunaepusha dosari ambazo zinaweza kujitokeza na kuathiri utekelezaji wa shughuli za uchaguzi,”alisema Jaji Mwambegele.
Alisema tume inaamini kuwa taasisi hizo zikishirikishwa vyema na wakapata uelewa wa kutosha kuhusu mchakato wa uchaguzi na itakuwa rahisi pia kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kupitia majukwaa yao kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Akizungumzia maandalizi alisema tume imeshafanya maandalizi mbalimbali ya uchaguzi mkuu hata hivyo ili zoezi hilo lifanikiwe kwakiwango kikubwa na kwamba inategemea sana ushirikiano kutoka katika taasisi za kiraia katika kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa uchaguzi.
Alisema katika kipindi cha vyama vya siasa vitapata fursa ya kuwanadi wagombea na kuelezea sera na ilani za uchaguzi za vyama vyao hivyo katika eneo hilo uzoefu unaonyesha kuwa kipindi cha kampeni kunakuqa na joto la kisiasa linalotokana na baadhi ya watu kukosa uvumilivu wa kisiasa hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa nchi.

“Kipindi hicho cha kampeni mnapaswa kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu kuwa makini kwa kuhakikisha kuwa hawawi chanzo cha kuvuruga amani na utulivu wa nchi yetu,”alisema Mwambegele.
Akizungumzia ratiba ya uchaguzi alisema Agosti 28 hadi Oktoba 28 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara.
Aliongeza tarehe 28 Agosti, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema na Tarehe 29 Oktoba, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndiyo Siku ya Kupiga Kura.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuwezesha Wanawake Kiuchumi na Afya ya Akili Francisca Mboya alisema kwao hii ni fursa ya kwakuwa tume imetuona kama daraja lakuunganisha wananchi katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Kutokana na takwimu zilizotolewa na INEC wiki hiiumla ya wapiga kura 37,655,559 wamejiandikisha na kuongeza kuwa idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwa kwenye daftari, mwaka 2020.

Kwa upande wa Zanzibar, Wapiga Kura 725,876 wapo katika Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.
Katika idadi ya wapiga kura 37,655,559 waliopo katika daftari, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapiga kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.
Kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69 na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu.

Jumla ya vituo 99,911 vitatumika kupigia kura ambapo vituo 97,349 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Bara na vituo 2,562 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar.
Idadi ya vituo 99,911 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020,” amesema.
