Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
SIKUmoja baada ya viongozi wa matawi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Kunduchi kuandamana hadi ofisi za chama hicho mkoa wa Dar es Salaam kulalamikia kukatwa kwa jina la aliyekuwa diwani wa kata hiyo Michael Urio, jina hilo limerejeshwa katika orodha ya wagombea.
Awali kabda ya kupitishwa majina hayo watia nia katika kata hiyo walikuwa zaidi ya watatu smbapo baada ya vikao yalirudishwa majina matatu ambayo miongoni mwao jina la Urio halikuwepo japokuwa alikuwa amepata kura nyingi katika uchaguzi.
Wanachama hao ambao inaelezwa kuwa maandamano yao yaliishia katika ofisi za chama mkoa ambapo walifanya mazungumzo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu jana lakini walionyesha kutoridhika na hatua hiyo.
Lakini Mtemvu aliwaahidi kuwa suala hilo lingeshughulikiwa na vikao vya chama vilivyoanza kufanyika leo na kesho.

Hatimaye, jioni ya leo jina la Urio limerejeshwa kwenye orodha ya watia nia ya kugombea nafasi ya udiwani Kata ya Kunduchi sambamba na majina ya kata zingine ambayo nayo hayakuwamo kwenye orodha iliyotolewa awali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Urio alithibitisha kurejeshwa kwa jina lake na kusema:
“Ni kweli jina limerudishwa, kwa sasa najiandaa na kampeni. Mengine ni mambo ya uchaguzi tu,” amesema Urio na kukata simu.
Mapema jana, ulienea uvumi kuwa jina la Urio halimo kati ya wateule wa nafasi hiyo kwa Kata ya Kunduchi, ambapo majina yaliyorejeshwa ni ya Happiness Kinyaha na Joyce Haule hali iliyozua sintofahamu kwa wafuasi wake.

