Na Asha Mwakyonde, DODOMA
MKURUGENZI Msaidizi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Abdulrahman Msham amewashauri watanzania kuwa na utaratibu wa kuandika wosia ili kuepusha migogoro ya mirathi katika baadhi ya familia.
Msham aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya wakulima maarufu Nane nane ambayo yanafanyika kitaifa Dodoma alisema kero nyingi ambazo wanazipokea tangu kuanza kwa Huduma ya msaada wa kisheria bure kupitia “Kampeni ya Mama Samia Legal Aid” nii katika eneo la mirathi.

Alieleza kuwa pamoja na kutatua migogoro katika eneo hilo la mirathi wamekuwa wakitoa ushauri wa namna ya kuandika wosia na kwamba changamoto nyingi walizozigundua ni watu wengi hawaandiki wosia.
Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema migogoro ya ardhi nayo imekuwa ni changamoto na kwamba wanaendelea kuitatua na kutoa elimu ya namna gani ya kutatuliwa kwa migogoro hiyo.

“Wizara ya Katiba inashiriki katika maonesho haya ya wakulima nane nane ambayo yanafanyika kitaifa Dodoma, nichukue nafasi hii kuwakaribisha wananchi wote kaufika katika viwanja hivi na kutembelea banda hili,” alisema.
Alifafanua kuwa wizara ya Katiba na Sheria ndio Wizara ambayo imepewa idhini ya kusimamia masuala yote ya haki huku akisema katika banda la Wizara hiyo wanatoa elimu ya kikatiba.

Aliongeza kuwa wananchi watakaofika katika banda hilo watapata elimu ya katiba na kufahamu sheria zote nchini ikiwamo ya uchaguzi.
Msham alisema kuwa wizara ya Katiba na Sheria pamoja na mambo mengine inatatua migogoro na kutoa elimu ya utatuzi kwa njia mbadala na elimu ya haki za binadamu, ulinzi wa mali asili na utajiri asilia wa nchi.
Aidha aliwakaribisha watanzania wote kufika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria kwa ajili ya kupata huduma na kwamba watakapofika watahudumiwa changamoto zao zote.
