WMA YAWAONYA WANAOWAPUNJA WAKULIMA

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

KAIMU Meneja wa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA),Mkoa wa Njombe, Henry Msambila, ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara na watu wote wanaojihusisha na udanganyifu wa vipimo kwa lengo la kuwapunja wakulima, akisema kuwa kitendo hicho ni kosa la jinai na adhabu yake ni faini ya kati ya shilingi 100,000 hadi milioni 20, au kifungo.

Akizungumza jana, Agosti 5, 2025, katika banda la WMA kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji Kitaifa (Nane Nane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, Msambila amesema kuwa serikali kupitia Wakala huo itaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kutumia vipimo visivyo halali.

Ameeleza kuwa tayari baadhi ya wahusika wamechukuliwa hatua na kwamba zoezi hilo ni endelevu, kwa kuwa jukumu kubwa la WMA ni kumlinda mkulima na mlaji kwa kuhakikisha matumizi ya vipimo sahihi.

“Tupo hapa kwenye maonesho haya kutoa elimu. Tunamlinda mkulima tangu ununuzi wa mbegu hadi kwenye mauzo ya mazao yake. Mbegu zote tunahakikisha ujazo wake ni sahihi,” alieleza Msambila.

Amefafanua kuwa WMA inahakiki bidhaa na mazao yaliyotokana na uzalishaji wa mkulima pamoja na vipimo anavyotumia kuuza, kwa lengo la kumwezesha kupata faida stahiki na kuepuka hasara.

“Tunamshauri mkulima asiuze kwa kutumia vifungashio vya kubuni au vipimo visivyo rasmi. Ni muhimu kutumia mizani halali, kwani kutumia vipimo batili ni hasara kwake na ni kosa kisheria,” amesema.

Msambila ameongeza kuwa wakala huo pia unahakiki vifungashio vinavyotumiwa na wakulima wanaoongeza thamani ya mazao, kwa kuhakikisha ujazo wa bidhaa unazingatia vipimo sahihi.

Aidha, aliwataka wananchi kutembelea banda la WMA kwenye maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu huduma na kazi mbalimbali zinazofanywa na wakala huo.