MGOMBEA URAIS CCM ACHUKUA FOMU KUGOMBEA KITI CHA URAIS 2025, APOKEWA KWA DUA NA MICHANGO YA WANANCHI CHAMWINO

Na Asha Mwakyonde, DODOMA

MGOMBEA wa kiti cha urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 9, 2025, amefika katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuchukua fomu ya kugombea urais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Rais Dk. Samia ameambatana na mgombea mwenza, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ambapo wote kwa pamoja walichukua fomu hiyo katika ofisi za INEC zilizopo Njedengwa, jijini Dodoma.

Kabla ya kufika INEC, Dk. Samia alipita kutoka Ikulu ya Chamwino na kusimamishwa na wananchi wa Wilaya ya Chamwino ambao walimpongeza, kumwombea dua na kumchangia kiasi cha shilingi 250,000 kwa ajili ya kuchukua fomu hiyo.

Akizungumza na wananchi hao, Rais Samia aliwashukuru kwa upendo na sapoti waliyoionyesha huku akiwataka waendelee kumuombea dua katika safari yake ya kuomba ridhaa ya kuiongoza tena Tanzania kupitia CCM.

“Nawashukuru kwa kuja kuniunga mkono katika safari hii inayoanza ya kwenda kukisemea chama chetu ili tupewe ridhaa ya kuendelea kukiongoza tena nchi yetu. Kwa hiyo leo tunakwenda kuchukua fomu, nikishaichukua nitarudi ili mnidhamini, tuanze rasmi safari ya kutafuta wadhamini,” alisema Rais Samia.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 umepangwa kufanyika Oktoba 29, mwaka huu.