NRA YAINGIA RASMI MBIO ZA URAIS, HASSAN ALMASI ATAJA NGUZO TATU ZA MATUMAINI

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MGOMBEA wa Urais kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), Hassan Almas, pamoja na Mgombea mwenza wake, Ally Hassan, leo Agosti 9, 2025, wamekuwa wa pili kuchukua fomu ya kugombea Urais katika Ofisi za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), zilizopo jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu, Almasi alisema kuwa hatua inayofuata sasa ni kutafuta wadhamini kutoka katika mikoa 10 ya Tanzania Bara kama inavyoelekezwa na sheria za uchaguzi.

Amesema baada ya hapo, wataelekeza nguvu kwa wapiga kura kwa ajili ya kuwasilisha ajenda za chama chao.

Katika maelezo yake, Almasi ameeleza kuwa wana matumaini makubwa katika safari hii ya uchaguzi, na akazitaja nguzo tatu kuu zinazowaongoza.

“Cha kwanza ni Mungu, maana yeye ndiye anayeshikilia uhai wetu na mamlaka yetu, nguzo ya pili ni wapiga kura kwa kuwa kikatiba wao ndio wenye mamlaka ya kuchagua uongozi wa nchi na nguzo ya tatu ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo ndiyo yenye dhamana ya kutangaza matokeo ya uchaguzi kwa haki na uwazi,” ameeleza.

Ameongeza kuwa hayo ndiyo matumaini makubwa wanayoyashikilia ili yawafikishe salama kwenye hatua nyingine ya mchakato huo.

Mgombea huyo amesema kuwa chama chao kinasisitiza kaulimbiu ya “Taifa kwanza, vyama baadaye”, akieleza kuwa wako tayari kukosa uongozi endapo hawatapewa ridhaa na wananchi na kwamba
si kuleta machafuko kwa sababu ya matokeo ya uchaguzi.

“Sisi tuko tayari kukosa uongozi endapo hatutaupata, lakini nchi ibaki salama. Hatuna sababu ya kuiingiza nchi kwenye machafuko kwa sababu ya uchaguzi. Baada ya uchaguzi kuna maisha, na Watanzania ndio wenye mamlaka ya kuweka uongozi wa taifa hili. Ndiyo maana nimetaja vitu vitatu: nchi, wapiga kura, na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambao ndio watatangaza matokeo,” alisema kwa msisitizo.

Wagombea hao waliwasili katika viwanja vya Ofisi ya Tume saa 1:55 asubuhi, wakiwa katika magari yenye namba za usajili T 964 ECB (aina ya Benz) na T 497 DNR (aina ya Murano).