Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
WANANCHI wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wameanza kunufaika na uboreshaji wa miundombinu kupitia Mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC), unaotekelezwa chini ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Songea, Wakili Bashir Muhoja, akizungumza manufaa ya mradi huo alisema awamu ya kwanza ya utekelezaji ni ujenzi wa barabara zenye urefu wa Km 10.01 kwa kiwango cha lami pamoja na ujenzi wa ofisi ya wahandisi itakayotumika kama maabara chini ya mkandarasi M/S CHINA SICHUAN INTERNATIONAL COOPERATION CO LTD kwa gharama ya shilingi bilioni 22.27.

Alisema kuwa awamu ya pili ina lenga kuboresha hali ya uchumi ya mji kwenye mapato ya halmashauri na wananchi kwa ujumla ambapo tayari mkandarasi ameshapatikana kwaajili ya ujenzi wa masoko makubwa mawili ya kisasa ya Manzese “A” ya kawaida, maduka ya kusimamia fedha, maghala, pamoja na kiwanda cha kuchakata mazao ya nafaka kwa gharama ya Sh. bilioni 22.9.
“Masoko haya yanakwenda kuongeza mapato ya halmashauri karibu Sh. bilioni 2, kwasasa tunakusanya Sh. bilioni 9 lakini ndani ya mwaka mmoja tutakuwa tunakusanya Sh. bilioni 11 kwa mwaka, tunamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwaajili ya kutekeleza miradi hii, pia nawaasa wananchi kutumia miundombinu hii kwa ufasaha kwa kuilinda na kuitunza ili iweze kudumu muda mrefu”.

Naye, Mhandisi Nicholaus Danda, Mratibu wa mradi wa TACTIC Manispaa ya Songea alisema barabara zote Km 10.01 zimejengwa katika kata za Mjini, Misufini, Majengo na Mfaranyaki ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2025 huku kazi zilizobaki ni kuweka alama za barabarani, kuziba mifereji, kuweka taa za barabarani na taa za kuongoza magari “traffic light” ambapo zikikamilika mandhari ya mji utabadilika hasa wakati wa usiku kwasababu ya taa.
Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Songea, Mhandisi Bakari John alieleza kuwa walikuwa wanatekeleza barabara za lami Km 2 tu lakini kupitia mradi wa TACTIC wameweza kutekeleza Km 10.01 ambapo imeleta matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu, kuboresha biashara na uchumi, kupunguza msongamano wa magari na kuboresha usalama wa watumiaji wa barabara katika mji wa Songea.

Naye Mtendaji wa Mtaa wa Matomondo, Editha Polisa, alisema kabla ya mradi, barabara zilikuwa na mashimo, wakati wa mvua maji yalikuwa yanaingia kwenye nyumba za watu lakini sasa wanaishukuru serikali kwa mradi, uchumi umeinuka nyumba zimepanda bei, thamani imeongezeka na wananchi wanazifikia huduma za kijamii na kiuchumi bila vikwazo ambapo wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuilinda miundombinu hiyo kwa kujiepusha kutupa taka kwenye mitaro ili isizibe na kuharibu barabara.

Vilevile, Mkazi wa Songea, Christopher Pata, anayejishughulisha na biashara ya kuuza chipsi aliishukuru serikali kwa barabara ya lami ambayo imewasaidia kuinua uchumi wao kwani bajaji, magari yanafika na wateja wameongezeka lakini kabla ya lami wateja walikuwa hawafiki njia ilikuwa na mashimo, vumbi na matope.
Mkazi mwingine wa Songea, Rashid Ally, dereva wa pikipiki ameeleza kuwa kipindi cha nyuma walikuwa wanatumia muda mrefu kuwapeleka wagonjwa hopitali ya Mjimwema kutokana na ubovu wa barabara, vyombo vyao vilikuwa vinaharibika lakini sasa hivi baada ya lami usafiri umekuwa mzuri na hata nauli imeshuka kutoka Sh. 2,000 hadi Sh. 1,000 au 1,500.
Naye, Hassan Pili Mkazi wa Songea aliishukuru serikali kwa ujenzi wa daraja la Matarawe kwasababu kipindi cha nyuma walikuwa wanavuka kwa shida kufuata huduma za kijamii na kiuchumi lakini sasa wanapita bila shida yoyote.
