Na Mwandishi Wetu,Dodoma
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa taarifa kwa umma kufuatia uvumi unaosambaa mitandaoni ukidai kwamba mfumo wa uchaguzi nchini umeunganishwa na mifumo mingine ikiwemo wa NIDA na chama kimoja cha siasa, na kwamba zoezi la kupiga kura tayari limekamilika.
Taarifa ya INEC imetolewa siku moja baada ya aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba,Humphrey Polepole ambapo alidai kuwa mfumo wa tume umeunganishwa na moja ya chama cha siasa nchini.
Tume imeeleza bayana kuwa taarifa hizo si za kweli, bali ni upotoshaji na uongo unaolenga kupotosha wananchi na kuleta taharuki katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu taarifa ya INEC iliyochapishwa leo na kusainiwa na Mkurugenzi Wa Uchaguzi, Ramadhani Kailima, hakuna mfumo wa kielektroniki unaotumika katika mchakato wa kupiga kura, kuhesabu kura au kutangaza matokeo. Uchaguzi wa Tanzania unafanyika kwa kutumia njia ya kawaida, ambapo kila mpiga kura hutambulishwa kwa kutumia Kadi ya Mpiga Kura iliyotolewa na Tume pekee.
Aidha, imeelezwa kuwa Kitambulisho cha Taifa (NIDA) hakitumiki kwa ajili ya kupiga kura, hivyo taarifa zinazoenezwa kuhusu matumizi yake katika uchaguzi ni za kupuuzwa.
Tume imefafanua pia kuwa baada ya kukamilika kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, vyama vyote vya siasa vilikabidhiwa nakala ya daftari hilo, ili kuhakikisha uwazi na ushirikishwaji wa wadau wote. Katika siku ya kupiga kura, mawakala wa vyama vya siasa hutumia daftari hilo kuthibitisha majina ya wapiga kura kwa kushirikiana na wasimamizi wa vituo. Hii ni hatua inayothibitisha kuwa mchakato wa uchaguzi unafanyika kwa uangalifu na kwa njia ya wazi bila kuhusisha mifumo ya siri au ya kielektroniki.
Kupitia taarifa hiyo, Tume imewasihi wananchi kuendelea kuwa watulivu na kutoamini taarifa zisizotolewa kupitia vyanzo rasmi. Imeeleza kuwa taarifa zote sahihi kuhusiana na mchakato wa uchaguzi zitapatikana kwenye tovuti rasmi ya Tume (www.inec.go.tz) pamoja na kurasa zake za mitandao ya kijamii.
Tume pia imeonya kwamba mtu yeyote anayeeneza upotoshaji ana lengo la kuleta taharuki kwa jamii, hivyo wananchi wanapaswa kuwapuuza na kuendelea kujiandaa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu ujao.
