Na Aziza Masoud,Dar es salaam
SERIKALI imesema ukosefu wa teknolojia za kisasa,takwimu sahihi na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika uchumi wa buluu ni changamoto kubwa katika sekta ya bahari hivyo imewataka wadau kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza leo Septemba 10, 2025 katika uzinduzi wa Kongamano la Uchumi wa Buluu lililoandaliwa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) linaloendelea jijini Dar es Salaam,Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Abdallah Mitawi alisema pamoja na mafanikio ya sekta ya bahari lakini bado ina changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa takwimu za kisasa na nyingine.

“Pamoja na mafanikio kuna changamoto ya ukosefu wa teknolojia za kisasa na takwimu sahihi,uelewa mdogo wa wananchi kuhusu fursa zilizopo katika uchumi wa buluu,”alisema Mitawi.
Alisema changamoto nyingine ni uvuvi haramu usioendelevu na uchafuzi wa mazingira ya baharini.

“Ni matumaini yangu kuwa kongamano hili litakuwa jukwaa la kuibua majawabu ya changamoto hizi, na pia kutoa mapendekezo ya kisera na kimkakati yatakayosaidia kuharakisha maendeleo ya sekta hii muhimu,”alisema Mitawi.
Alisema kuwa kupitia kongamano hilo wahusika wataweza kuona fursa na rasilimali zilizopo baharini ambapo zikitumika ipasavyo zina uwezo wa kuongeza ajira kwa vijana kuchochea biashara na usafirishaji,kukuza utalii wa bahari na fukwe,kukuza uvuvi na usalama wa chakula pamoja na kukuza nishati jadidifu na utafiti wa kisayansi.

“Kongamano hili limeleta wataalamu mbalimbali watakaojadili kwa kina namna ya kuchangamkia fursa zilizopo katika Sekta hii ya Uchumi wa Buluu kwa kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira, kwa kufanya hivyo itawezesha uendelevu wa rasilimali zetu na vizazi vya sasa na vijavyo vinufaike na rasilimali zetu za Uchumi wa buluu,”alisema Mitawi.
Akizungumzia kuhusu kuboresha uchumi wa buluu alisema katika kipindi cha miaka michache iliyopita, Serikali kupitia sera na mipango mbalimbali imeweka msisitizo mkubwa kwenye maendeleo ya uchumi wa buluu.

Alisema sera hiyo ni pamoja na kuboreshwa kwa miundombinu ya bandari,uimarishaji wa sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.
“Mipango mingine ni kuwekezwa katika utafiti wa kisayansi kuhusu bahari zetu,kanzishwa kwa miongozo ya usalama wa baharini na uhifadhi wa mazingira ya majini na Kuimarishwa kwa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya bahari,”alisema Mitawi.

Alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali kubwa na nyingi za uchumi wa buluu ikiwemo Kilomita za mraba 64,000 za bahari ya kitaifa Kilomita za mraba 223,000 za Ukanda wa Kiuchumi wa Kipekee (EEZ),Pwani yenye urefu wa kilomita 1,424 ambayo ni muhimu kwa shughuli za uvuvi, ufugaji wa samaki baharini, na utalii.
“Tanzania ina Kilomita za mraba 61,500 za maji baridi zinazofaa kwa matumizi mbalimbali na zinazoweza kutoa takriban mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka; Eneo la hekta milioni 29.4 linalofaa kwa umwagiliaji.

“Misitu ya Pwani inayokadiriwa kufunika eneo la kilomita za mraba 700; Kilomita za mraba takribani 1,440 kwa taarifa za nyuma (158,100 National Mangrove Management and Development Strategy 2025 – 2035 kwa taarifa za mkakati tajwa) za Misitu ya mikoko, Kilomita za mraba 3,580 za miamba ya matumbawe; Kilomita za mraba 307,800 za maeneo ya hifadhi sawa na asilimia 32.5 ya eneo lote la nchi,”alisema Mitawi.
Alisema takriban samaki wa maji chumvi aina 33 na aina 17 za samaki wa maji baridi zinazoweza kuvunwa; Akiba ya gesi asilia baharini inayokadiriwa kuwa futi za ujazo trilioni 47.13; na Bandari rasmi 86 na bandari zisizo rasmi 885 zinazotumika kusafirisha mizigo mbalimbali yenye bidhaa tofauti.

“Napenda kutambua kwa dhati Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa mchango wake mkubwa katika kutoa elimu ya bahari, kufanya tafiti bunifu, na kutoa mafunzo ya vitendo kwa ajili ya sekta ya bahari na uchumi wa buluu.
“Uchumi wa buluu ni dhana inayojumuisha matumizi endelevu ya rasilimali za bahari, maziwa, mito, ardhi oevu na maji chini ya ardhi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi, kuboresha maisha ya watu, na kuhakikisha uendelevu wa mazingira ya baharini unazingatiwa,”alisema.

Awali Mkuu wa chuo cha DMI Profesa Tumaini Gurumo alisema kongamano la uchumi wa Buluu limekutanisha wadau wa uchumi wa buluu ambao kiuhalisia ni wengi mno kwakuwa uchumi wa buluu unagusa kila wizara zikiwemo za kilimo,uvuvi,uchukuzi na wizara nyingine.
“Lengo kuu la kongamano letu ni kujadili nakufanya tathimini ya maendeleo ya buluu Tanzania,tumejikita kutazama kuanzia 2021 mpaka mwaka huu,tunaangalia niini kimefanyika lakini pia tunaangalia kama kuna changamoto ili tuangalie namna zilivyopata utatuzi lakini pia ambazo hazijapata utatuzi tunazitatuaje,”alisema Profesa Gurumo.

Alisema kongamano la uchumi wa buluu pia limeingia katika dira 2050 kwa lengo la kuinua sekta hiyo.
Alisema kongamano hilo la siku mbili lina kauli mbiyu bahari yetu,fursa zetu,wajibu wetu.

Kongamano hili linafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Wizara ya Uchukuzi kupitia Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) pamoja na Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi – Zanzibar.
