MPINA AKATAA GARI LA INEC

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MGOMBEA urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya hiyo leo, Septemba 13, 2025, katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), huku akitoa msimamo wa kipekee wa kukataa gari la kampeni aina ya Landcruiser linalotolewa na tume hiyo kwa wagombea.

Mpina amekuwa mgombea wa kwanza kati ya wagombea 17 waliojitokeza kugombea urais kukataa usafiri huo, wakati wagombea wengine 16 tayari wamepokea magari hayo na kuanza kuyatumia kwenye kampeni zao.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Mwanasheria wa ACT-Wazalendo, Omari Said Shabani, alisema chama hicho hakina changamoto upande wa usafiri na kilichoomba kwa tume ni kuhakikisha kinalindwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.

“Tunashukuru kwa ofa ya magari, lakini ACT-Wazalendo tumejipanga na tunajitosheleza kwa usafiri wa kampeni. Tunaiomba INEC ihakikishe ulinzi kwa mgombea wetu na timu yake, hilo ndilo muhimu zaidi kwetu,” alisema Shabani.

Uamuzi huo umeibua mjadala wa kisiasa, baadhi ya wachambuzi wakisema unaleta taswira ya chama chenye kujiamini, huku wengine wakitafsiri kama mkakati wa kuonesha tofauti ya ACT-Wazalendo na vyama vingine katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mpina amechukua fomu leo baada ya kushinda kesi aliyoifungulia dhidi ya INEC ambapo alipinga kuenguliwa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais Agosti 26.