REA YATOA MAFUNZO YA NISHATI SAFI KWA MAKUNDI MAALUM

Mwandishi Wetu Katavi

WAKALA wa Nishati Vijijini (REA), imepongezwa kwa kuwezesha na kuhamasisha upatikanaji wa nishati bora na salama kwa wananchi walioko maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji ili watanzania watumie nishati safi na salama nchini.

Pongezi hizo zimetolewa leo Oktoba 23, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuf wakati akifungua mafunzo ya elimu ya matumizi ya nishati safi kwa Makindi Maalum iliyofanyika mkoani Katavi.

Mhe. Yusuf amewapongeza pia TAMAVITA (Taasisi ya Maendeleo kwa Viziwi Tanzania) kwa kushirikiana na REA katika uhamasishaji na kukubali kupewa mafunzo hayo kutoka REA ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa, Rais Samia ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi nchini na kuwapongeza TAMAVITA kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhama kutoka kwenye matumizi ya nishati zisizo safi na salama na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia.

Amesema matumizi ya nishati zisizo safi zinamadhara kwa afya ya binaadamu kupitia joto na moshi unaotokana na nishati hizo ambao unatoa kemikali ambayo sio salama kwa afya hivyo kila mmoja abadilike na amhamasishe mwingine katika hilo.

Naye, Mhandisi kutoka REA, Ramadhan Mganga amesema kuwa Wakala umeandaa mpango maalum wa kuwezesha taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 100 kwa siku kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Tunataka ifikapo mwaka 2034; 80% ya Watanzania wawe wanatumia Nishati Safi ya Kupikia, kwa manufaa yao na vizazi vijavyo,” amesisitiza Mha. Mganga.

Kwa upande wake, Meneja wa Bishara kutoka Tango Energy Limited, Sunday Nyembele amesema kuwa jumla ya majiko banifu 60 yatauzws kwa TAMAVITA katika semina hiyo na majiko banifu 3,126 yatauzwa kwa wananchi wa mkoa wa Katavi.

TAMAVITA ni taasisi maalum kwa walemavu wasiosikia viziwi inayojushughulisha na shughuli za ujasiliamali pamoja na utoaji wa elimu mbalimbali katika jamii ya walemavu viziwi.