OTHMAN:NITAREJESSHA HADHI YA ZANZIBAR DUNIANI

Na Mwandishi Wetu,ChakeChake

MGOMBEA urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amesema atahakikisha Zanzibar inarejesha hadhi na heshima yake katika jumuiya ya kimataifa mara baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar.

Akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kufunga kampeni uliofanyika Viwanja vya Tibirizi, Chake Chake Pemba, Othman alisema Zanzibar ilikuwa na historia ya kujitawala na kutambulika kimataifa, hivyo ni wakati wa kuirudisha kwenye nafasi hiyo ya kiheshima.

“Haiwezekani watu kuingia ovyo Zanzibar bila taratibu, na haki za Zanzibar ndani ya Muungano lazima zipatikane. Tunataka Zanzibar yenye mamlaka yake kamili na inayoheshimika duniani,” alisema Othman huku akishangiliwa na wafuasi wake.

Aliongeza kuwa serikali itakayoongozwa na ACT Wazalendo itasimamia maslahi ya wananchi, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha haki za Zanzibar ndani ya Muungano zinaheshimiwa.

Othman pia alitumia mkutano huo kuwataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kufanya uamuzi wa kuiletea Zanzibar mwelekeo mpya wa maendeleo na heshima.