Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam
WIZARA ya Uchukuzi imewataka wahitimu na wadau mbalimbali wa sekta ya uchukuzi kupanga mipango yao kulingana na Dira 2050 yenye lengo la kukuza uchumi wa buluu kupitia sekta ya usafirishaji funganishi.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile katika mahafali ya 21 ya Chuo Cha Bahari Dar es Salaam (DMI),alisema ni wakati wa nchi kutumia rasilimali zake hasa watalaam wanaotokana na chuo hicho kufikia malengo na matarajio ya kukuza uchumi wa buluu nchini.

Alisema wakati Taifa linapoendelea kujijengea uwezo wa ndani hasa katika maandalizi ya rasilimali watu sekta ya uchukuzi kuwa Dira 2050 imeweka matarajio mbalimbali ambayo hawana budi kuyafanyia kazi kuyafikia matarajio.
Alisema matarajio hayo ni pamoja na Tanzania kuwa lango kuu la biashara mashariki na kusini mwa Afrika ikitumia nafasi yake ya kijiografia kurahisisha biashara mipakani na kuimarisha ushirikiano.

“Matarajio mengine niTaifa linaloongoza kwa biashara ya usafirishaji likiunganisha nchi za Afrika Mashariki, za kati na kusini na masoko mengine ya kimataifa,”alisema Kihenzile.
Alisema pia matarajio mengine kuwa na mtandao wa usafirishaji fungamanishi wenye mfumo wa kisasa na shindani, unaounganisha shoroba za kiuchumi ili kuwezesha biashara za ndani na za kimataifa kwa ufanisi na kuongeza ushindani wa Tanzania katika sekta ya usafirishaji.

“Pia tunapaswa kuwa na watoa huduma za usafirishaji wenye viwango vya kimataifa, wenye kutoa huduma kwa ushindani huku wakitumia teknolojia za kisasa za kidijitali ili kuongeza ufanisi na kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa katika mnyororo wa thamani,”alisema Kihenzile.
Alisema Dira 2050 pia imepanga kuwa mazingira bora ya usimamizi wa usafirishaji yanayorahisisha taratibu za forodha, kupunguza urasimu na vikwazo, kuzingatia viwango vya kimataifa, na kuendana na kasi ya maendeleo katika sekta ya usafirishaji.

“Uwepo wa mtandao jumuishi wa usafirishaji wenye miundombinu inayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ili kutoa fursa sawa kwa wote katika biashara za ndani na kimataifa,”alisema Kihenzile.
Awali Mkuu wa chuo DMI Profesa Tumaini Gurumo alisema katika mahafali haya jumla ya wanafunzi 2076 wamefuzu na kuidhinishwa na Baraza la Taaluma kutunukiwa vyeti kulingana na maeneo waliyofuzu.
“Miongoni mwao wapo wanafunzi 78 wa Shahada ya Uzamili, 592 wa Shahada, 374 wa Stashahada, 446 wa Astashahada, 538 wa Astashahada ya Awali. Wanafunzi 48 wa vyeti vya umahiri (CoC) wakiwemo Manahodha na Wahandisi Meli 17 wa daraja la 2/1, 22 wa daraja la 3, 7 wa daraja la 4 na maafisa umeme melini wawili. Kati yao Wanawake wako 512 ambao ni asilimia 24,”alisema Profesa Gurumo.

Alisema chuo kina programu kumi (10) za umahiri kwa maafisa wa Meli, kozi sita (6) za kitaaluma kwa ngazi Shahada ya Uzamili, tisa (9) kwa ngazi ya Shahada, tisa (9) kwa ngazi ya Stashahada, tisa (9) kwa ngazi ya Astashahada na zaidi ya Hamsini (50) kwa kozi fupi.
“Chuo kimeendelea kuongeza programu mpya kulingana na mahitaji ya ukuaji wa sekta hususan mahitaji ya rasilimali watu;kufanya tafiti pamoja na kutumia wataalamu wa sekta ya bahari wabobezi waliopo katika Chuo cha Bahari Dar es Salaam kutoa ushauri elekezi kwa taasisi za Umma na taasisi binafsi,”alisema Profesa Gurumo.


