TRA YAKUSANYA SH TRILIONI 4.13 DESEMBA YAVUKA LENGO LA MAKUSANYO 

Na Mwandishi Wetu,Dar es Salaam 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuvunja rekodi yake ya ukusanyaji wa wa mapato yatokanayo na kodi  ambapo kwa mwezi Desemba pekee imekusanya   Sh. Trilioni 4.13 kwa sawa na ufanisi wa asilimia 102.9 ya lengo ambalo lilikuwa ni kukusanya Sh. Trilioni 4.01.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Januari 1, 2026  Kamishna Mkuu wa TRA  Yusuph  Mwenda amesema katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba TRA imekusanya kiasi cha Sh.  Trilioni 9.8 sawa na ufanisi wa asilimia 101.45 ya lengo la kukusanya Sh. Trilioni 9.66.

“Katika ukusanyaji huo wa robo mwaka mwezi Desemba pekee tumekusanya   Sh. Trilioni 4.13 kwa sawa na ufanisi wa asilimia 102.9 ya lengo ambalo lilikuwa ni kukusanya Sh. Trilioni 4.01,”alisema Mwenda.

Amesema makusanyo hayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 12.26 toka Sh. Trilioni 8.73 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho mwaka 2024/2025 ambapo ongezeko la makusanyo hayo ya kodi limetokana na kuongezeka kwa ulipaji kodi kwa hiari nchini.

Kamishna Mkuu Mwenda amesema tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026 TRA imevuka malengo ya makusanyo kwa kila mwezi jambo ambalo limesababishwa na uhimilivu wa shughuli za uchumi uliojengwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

“Mhe. Rais amejenga uhimilivu wa shughuli za uchumi ambao umeonyesha matokeo katika makusanyo ya kodi na miongozo ambayo tumekuwa tukipewa na Serikali ya awamu ya sita imeonyesha kuwa na matunda” amesema Mwenda. 

Amesema kuwa wastani wa makusanyo kwa mwezi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2025/2026 umefikia Sh. Trilioni 3.13 ambacho ni kiasi cha juu kabisa ukilinganisha na Wastani wa Sh. Trilioni 2.75 kwa kipindi kama hicho mwaka 2024/2025.

Ametaja sababu nyingine zilizoongeza makusanyo kuwa ni kuendeleza ushirikiano na wafanyabiashara pamoja na vyama vya wafanyabiashara, kuendelea kuboresha mahusiano na Walipakodi na kuendelea kusimamia utendaji mzuri, nidhamu na kuchochea ubunifu. 

Kuendelea kuhimiza utatuzi wa migogoro ya kikodi kwa njia ya majadiliano na makubaliano ya nje ya mahakama nako kumeongeza mapato maana katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2025 kulikuwa na makubaliano maalum 42 yenye thamani ya kodi ya Sh. Bilioni 9.4.

“Kuendelea kufuatilia kwa karibu hali ya ufanyaji biashara nchini kwa kusimamia kikamilifu uzalishaji wa viwandani pamoja na kuendelea kuhimiza matumizi ya mashine za kielektroniki.