DK.NCHEMBA:BWAWA LA MAJI KIDUNDA SULUHU YA KUDUMU MTO RUVU

Na Mwandishi Wetu,Morogoro

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa la kuhifadhi maji la Kidunda na kubainisha kuwa kukamilika kwa mradi huo wa bilioni 336 kutachochea ukuaji wa maendeleo ya jamii kwa wakazi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Dkt. Mwigulu amebainisha uwekezaji wa mradi huo utakavyosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam haswa katika msimu wa kiangazi.

Aidha Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati ukiwepo mradi wa kidunda unaotekelezwa katika Kata ya Mkulazi mkoani Morogoro.

“Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha fedha zaidi ya bilioni 336 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu wenye manufaa makubwa kwa mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Pwani, ambapo angeweza kutekeleza miradi mingine lakini hakusita kuweka fedha kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji,” amesema Dkt. Mwigulu

Pia ametoa wito kwa wizara ya fedha kutoa ushirikiano wa kuhakikisha fedha inayohitajika kukamilisha mradi wa Kidunda inatolewa kwa wakati ili lengo lililowekwa na Serikali liweze kufikia na kuondosha changamoto ya huduma ya maji kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

“Nitoe maelekezo kwa wizara ya fedha, kuwapa ushirikiano kwa wizara ya maji kuhakikisha mradi huu unakamilika ifikapo mwezi Disemba 2026 kama ilivyoelekezwa, kwa maana kukamilika kwake hatutapata tena changamoto za kukosekana kwa maji kwenye mikoa hii iliyopata shida kupitia mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Dkt. Mwigulu.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mheshimiwa Jumaa Aweso (Mb) amesema mradi wa Kidunda unategemewa kutoa hatma ya upungufu wa maji wakati wa kiangazi ambapo unatarajiwa kuhifadhi maji kiasi cha lita milioni 190 kwa mwaka na kuwezesha mitambo ya kuzalisha maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini kuzalisha maji kwa mwaka mzima bila changamoto yeyote.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuidhinisha fedha za awali takribani bilioni 100 zilizomsaidia mkandarasi kuanza mwezi wa sita mwaka 2025 na ambapo tunategemea utekelezaji utafanyika kwa kasi, tuna uhakika mradi utakamilika kwa wakati uliowekwa kimkataba,” amesema Mheshimiwa Aweso

Aidha ziara hii ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Waziri wa Uchukuzi, Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Nishati, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mazingira, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro sambamba na Wabunge.