Na Asha Mwakyonde, DODOMA
WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya marekebisho ya Kanuni za Ushirikishwaji wa Watanzania za mwaka 2018 ambapo Tume hiyo mara kwa mara itatangaza kupitia Kanuni ya 13A orodha ya bidhaa na huduma ambazo zinatakiwa kutolewa na kampuni za Kitanzania ambazo zinamilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania , lengo likiwa ni kuongeza wigo wa ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini kwa manufaa mapana ya taifa.
Pia ametoa rai kwa Watanzania,
kuendelea kuhakikisha wanapata utaalamu sahihi unaohitajika katika
shughuli za madini ili kuweza kuwa miongoni mwa wanaostahili kupatiwa fursa za ajira katika migodi sambamba na fursa za utoaji huduma katika miradi hiyo.
Hayo aliyasema jana jijini hapa wakati akizungumza na waandishi wa habari alisema kwa awamu ya kwanza Novemba 14 2025 ambapo Tume ya Madini
ilitangaza orodha ya bidhaa na huduma zinazotakiwa kutolewa na
kampuni zinazomilikiwa na kampuni za kitanzania kwa asilimia 100.
Alieleza kuwa watoa huduma wote wahakikishe wanatoa huduma
bora kulingana na viwango stahiki ili kuendelea kuaminika katika utoaji wa huduma husika.

“Niwasisitize wawekezaji wote
kuzingatia Sheria ya Madini Sura 123 na utekelezaji wa Kanuni za Local Content sambamba na kuwataka Watanzania kuchangamkia fursa
mbalimbali zilizopo katika miradi ya madini ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa manufaa ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mavunde.
Aliongeza kuwa Wizara ya Madini inaahidi kuendelea kuwapa ushirikiano wawekezaji wote
wa ndani na nje ya nchi wenye nia ya kufanya uwekezaji wenye tija na
kukuza uchumi wa taifa letu kutokana na uvunaji wa rasilimali madini.
Waziri Mavunde alifafanua kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeendelea kuhakikisha rasilimali madini inakuwa na manufaa kwa Watanzania wote kupitia makusanyo ya moja kwa moja yatokanayo na shughuli mbalimbali za madini, kuhakikisha uwepo wa fursa za ajira kwa Watanzania kupitia taaluma na ujuzi walio nao pamoja na utoaji wa huduma katika miradi ya madini,na ununuzi katika migodi unafanyika kwa kutoa kipaumbele kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.

Alisema kutokana na jitihada hizo, mapato ya Serikali
yameendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 526.722 sawa na asilimia 111 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2020/2021 hadi kufikia kiasi cha Shilingi trilioni 1.071 sawa na asilimia 107.13 ya lengo la makusanyo kwa mwaka 2024/2025.
Aidha, Mavunde aliongeza kwa mwaka 2025/2026 Wizara imewekewa lengo la kukusanya kiasi cha Shilingi trilioni 1.2 ambapo katika kipindi cha miezi sita, kuanzia Julai, 2025 hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2025, jumla ya kiasi cha Shilingi bilioni 653.139 kimekusanywa sawa na asilimia 108.86 ya lengo la kukusanya Shilingi bilioni 600 kwa kipindi husika na sawa na asilimia 54.42 ya lengo la mwaka.


