COPRA YAGAWA MBEGU ZA MBAAZI KWA WAKULIMA DODOMA

Na Asha Mwakyonde, Dodoma

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA) leo imekabidhi tani 2.5 za mbegu za mbaazi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kwa lengo la kuwanufaisha wakulima wa Halmashauri za Chemba, Kondoa na Kongwa wanaotumia mfumo wa Stakabadhi za Ghala kuuza mazao yao.

Akizungumza Januari 6, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi mbegu hizo, Mkuu wa Mkoa Senyamule amewahimiza wakulima kuuza mazao yao kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala, akisisitiza viongozi wa wilaya kuwahamasisha wananchi kujenga maghala na kuyasimamia ipasavyo ili wakulima wengi zaidi wanufaike na mfumo huo.

Amesema mfumo wa Stakabadhi za Ghala ndiyo mwelekeo na njia rasmi ya Serikali katika uuzaji wa mazao ya kilimo nchini.
Ameeleza kuwa kugawa mbegu za mbaazi bure kwa wakulima ni historia mpya kwa Mkoa wa Dodoma, kwani ni mara ya kwanza tukio hilo kufanyika.

“Hii ni historia nyingine ambayo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameivunja katika sekta ya kilimo. Nawapongeza COPRA pamoja na taasisi zote zinazohusika na mfumo wa Stakabadhi za Ghala,” amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa Mkoa wa Dodoma haukuwa umeanza kutumia mfumo huo kikamilifu hadi msimu wa mwaka 2023/2024, ambapo ulianza kutumika kwa mazao machache yakiwemo mbaazi, ufuta na dengu.

“Tunaongelea jambo ambalo halikuwahi kufanyika. Leo ndiyo mwanzo wake. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan bado ana maono makubwa na mazuri kwa ajili ya wakulima wa nchi yetu,” amesema.

Aidha, amewapongeza wakulima kwa kuuelewa na kuanza kunufaika na mfumo wa Stakabadhi za Ghala, akisema mwaka huu wameanza kushuhudia manufaa makubwa yanayotokana na mfumo huo.

Awali, Mkuu wa Kanda ya Kati kutoka COPRA, Andrew Mgaya, amesema kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa COPRA wamekabidhi mbegu hizo huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa juhudi zake za kuhakikisha mbaazi na mazao mengine yanaingizwa kwenye mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Ameeleza kuwa uingizwaji wa mbaazi na mazao mengine katika mfumo huo umeanza kuzaa matunda, ikiwa ni pamoja na uwepo wa shilingi 30 katika muundo wa bei kwa ajili ya uendelezaji wa mazao.

“Fedha hizo hutumika kununua mbegu, kuwapatia wakulima, kununua viuatilifu na kufanya tafiti mbalimbali zinazohitajika katika uzalishaji wa mazao,” amesema.
Mgaya pia amemuomba Mkuu wa Mkoa kuwahimiza viongozi wa wilaya kuhakikisha mazao ya choroko, dengu, mbaazi na ufuta yanauzwa kupitia mfumo wa Stakabadhi za Ghala.

Amefafanua kuwa mazao hayo yakiuzwa kupitia mfumo huo, wakulima watanufaika kwa kupata mbegu nyingi zaidi msimu ujao, huku akisisitiza kuwa COPRA ina fedha za kununua mazao hayo.